ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, November 24, 2021

SERIKALI KUFANYA UCHUNGUZI KUPANDA KWA BEI YA SARUJI.

 


Serikali ya Tanzania imeiagiza Tume ya Ushindani wa Biashara Nchini (FCC) kufanya uchunguzi kuhusiana na kupanda kwa bei ya saruji nchini.

Agizo hilo limetolewa leo Jumatano na Novemba 24, 2021 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo wakati akizungumzia hatua wanazochukua baada ya kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi nchini.

Amesema wizara hiyo imefanya tathimini ya bei ya bidhaa za saruji, mabati na nondo katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza, Pwani, Shinyanga na Ruvuma.

Amesema tathimini hiyo ya mwenendo wa bei iliangalia bei za bidhaa hizo kati ya Septemba hadi Novemba mwaka huu kwenye mikoa hiyo na kubaini kuwa bei ya saruji ilipanda kwa wastani wa Sh1000 kwa kila mfuko wa kilo 50.

Kwa upande wa mabati tathimini hiyo ilionyesha kuwa imepanda kwa wastani wa asilimia 5.5 kwa mabati ya gauge 28.

Profesa Mkumbo amesema kwa upande wa nondo zimepanda kwa wastani wa asilimia sita katika kipindi hicho.

“Kupanda kwa bei za saruji katika kipindi cha tathimini kulisababishwa na mfumo wa usambazaji wa bidhaa hiyo na hakukutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji viwandani,”amesema.

Amesema kutokana na hivyo ongezeko la saruji katika kipindi hicho tajwa linachukuliwa kuwa halikuwa halali na hivyo Serikali imeiagiza FCC kuchunguza na kuchukua hatua.

Hata hivyo, amesema kuongezeka kwa bei za bidhaa zinatokana na malighafi ya vyuma (mabati na nondo) kulikotokana na kupanda kwa bei za malighafi kutoka nje kwa kuwa malighafi za bidhaa hizo kutoka ndani hazitoshelezi.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.