Na Atley Kuni, WAMJW- DSM.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia wazee na Watoto, Mhe. Dorothy Gwajima, amesema Tanzania imepiga hatua katika Sekta ya Afya, hususan kwenye huduma za Mama na Mtoto ambapo idadi ya akina mama wajawazito wanaohudhuria kliniki imeongezeka na kufikia asilimia 83 kwa mwaka 2021 ikilinganishwa na asilimia 58 ya mwaka 2015.
Akifungua Mkutano wa 22 wa Mapitio ya Sera na mafanikio kwenye Sekta ya Afya,Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima amesema, lengo lilikuwa kufikia asilimia 80 ya mahudhurio manne ya kliniki lakini kutokana na uboreshaji wa sehemu za kutolea huduma za Afya, imewezesha kuongeza mahudhurio na kufikia mahudhurio manne ambayo ni zaidi ya malengo.
“Mikoa vinara kwa kina mama wengi kuwa na mwamko wa kwenda kliniki ni Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mtwara, Iringa, Lindi na Njombe, Mikoa mingine mnapaswa kuiga mfano huo kwa kujifunza na nikujua ni mbinu zipi mikoa hiyo imetumia na kufanikiwa ili wengine muweze kutekeleza kwenye Mikoa yenu” Amesema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima, amesema kwa sasa Serikali katika ngazi ya Msingi imefanikisha kusajili zahanati 5,325, vituo vya afya 629 pamoja na Hospitali za Wilaya 68 ambazo zote zinatoa huduma, aidha vituo 415 vinatoa huduma ya dharura ya upasuaji kwa mama wajawazito na huduma kwa Watoto wachanga hali iliyoongeza mwamko kwa kina mama kwenda vituoni pindi wawapo wajawazito.
Kuhusiana na suala la Uviko-19, Dkt. Gwajima, amesema, Serikali imeweza kufanyia kazi mapendekezo kumi na tisa yaliyo tolewa Mei 17, 2021 na kamati kitaifa ya kumshauri Rais, kuhusu mwenendo wa Uviko hapa nchini.
“Tanzania kama zilivyo nchi zingine inazingatia chanjo kama afua muhimu ambapo kupitia COVAX facility imetengewa chanjo 12,049,827 na hadi sasa imepokea za chanjo 1,223,400 aina ya Janssen, Sinopharm chanjo 1,065,600 na chanjo aina ya Pfizer 500,000 tulizo pokelewa mapema Novemba, 23, 2021.´Amesema Gwajima.
Dkt. Gwajima, ametumia fursa hiyo kuwashukuru watu wa kada zote kwa namna walivyo simama kidete katika kuelimisha na kuhamasisha afua ya chanjo wakiwepo waandishi wa Habari, viongozi wa kisiasa, viongozi wa kidini Pamoja na makundi yote katika utumishi wa umma.
Awali akimkaribisha Waziri Gwajima kutoa Hotuba yake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI) Dkt Festo Dugange, alisema hadi kufikia mwezi Novemba, 2021 Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipeleka fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 55.25 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 221 katika maeneo ya kimkakati kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Aidha kuhusu Mapambano dhidi ya UVIKO-19 “Serikali imeweza kununua Vifaa Tiba vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 95.37 kupitia fedha ya mkopo nafuu wa IMF kwa ajili ya Vituo vya kutolea huduma za Afya katika ngazi ya Halmashauri” Amesema Dugange na kuongeza,
“Halmashauri zinaendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya majengo ya Idara ya dharura (EMD)-80, Wagonjwa mahututi (ICU) - 26, Nyumba za Watumishi 150 katika Vituo vya kutolea huduma za Afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa gharama ya Shilingi bilioni 44.5 kupitia fedha hizo hizo za IMF haya ni mapinduzi makubwa sana katika Sekta ya Afya, alisisitiza Dugange.
Akitoa wasilisho kwenye Mkutano huo wa Mwaka wa tathmini, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe, amesema Serikali kwa sasa pamoja na mambo mengine inafanya uimarishaji wa mifumo ya TEHAMA, kwani mifumo kama Afya Care na GoTHOMIS, ambayo itasaidia kuimarisha takwimu za afya lakini pia kuwa na mipango inayopimika kwakuweka vipaumbele kulingana na takwimu wanazo zipata kwenye mifumo hiyo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.