ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, December 29, 2019

MPINA AVUNJA MKATABA ULIOINGIZA SERIKALI HASARA YA BILIONI 15, AAGIZA VIGOGO NARCO, TMCL, NICOL KUCHUKULIWA HATUA KALI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina akizungumza na wafanyakazi wa machinjio ya Dodoma wakati akitangaza kuvunja mkataba baina ya Kampuni ya NICOL na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) iliyokuwa ikiendesha kwa ubia Kampuni ya TMCL ambayo imetwaliwa na Serikali. Picha na Mpiga Picha  

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amevunja mkataba wa mauzo ya mali za machinjio ya Dodoma baina ya Serikali na Kampuni ya NICOL  na kuirejesha machinjio hiyo chini ya umiliki wa Serikali baada ya kuwepo kashfa ya ufisadi wa shilingi bilioni 15, usimamizi mbovu, ubadhirifu na ukiukwaji mkubwa wa mkataba uendeshaji wa machinjio hiyo.

Hivyo NICOL imetakiwa kulipa kiasi cha jumla ya shilingi 9,712,127,660 ambazo Serikali ilipunjwa katika biashara ya machinjio. Pia Serikali imeitaka NICOL kulipa madeni yote inayodaiwa Kampuni ya Ubia TMCL kiasi cha shilingi 5,248,084,000.
Akitangaza uamuzi huo wa Serikali mbele ya wafanyakazi wa Kampuni ya TMCL Kizota jijini Dodoma, Waziri Mpina alisema mkataba huo uliosaniwa Mwaka 2008 umevunjwa kwa kuzingatia Ibara ya 7 na ya 13 ya Mkataba wa Mauzo ya Mali (Asset Sale Agreement), Hivyo, kuanzia sasa Machinjio yametwaliwa na Serikali baada ya kubainika kasoro nyingi.
Pia Waziri Mpina ameitaka Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambaye ni mbia katika Kampuni ya Ubia TMCL kujiondoa ndani ya siku 60 kuanzia jana kwani kampuni ya Serikali haiwezi kushiriki uhalifu na hujuma kubwa kiwango hicho.
Kufuatia Kashfa hiyo Serikali imeviagiza vyombo vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua za kisheria watendaji wote wa NICOL, NARCO na TMCL waliohusika na ubadhirifu wa mali za Kampuni ya TMCL na kuisababishia hasara Serikali tangu mwaka 2008 hadi sasa.
Hivyo Waziri Mpina ameelekeza huduma za uchinjaji zitaendelea kutolewa kama kawaida katika kipindi cha mpito chini ya usimamizi wa Serikali wakati mchakato wa kumpata mwekezaji mahiri wa mpito na wa kudumu unaendelea ambapo Serikali imemteua Victor Mwita kuwa Kaimu Meneja wa Machinjio ya Dodoma.
Waziri Mpina amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambayo imejipambanua kuwa ni Serikali ya Viwanda na Serikali ya wanyonge haitakubali hujuma na ufisadi uliokuwa ukifanyika katika Machinjio ya Dodoma uendelee.

Aidha amewahakikishia watanzania kuwa wote waliohusika na wizi na ubadhirifu hawatapona kwani Serikali inajua kuwa hata mishahara ya wafanyakazi nayo ilifanyiwa ufisadi na kuleta usumbufu mkubwa.

“Pia tunatambua mahitaji ya uchinjaji mifugo na kusafirisha nyama nje ya nchi ambapo kusimama kwa Machinjio hii kulisababisha wafugaji na vijana wengi kukosa ajira na masoko ya uhakika”alisema Waziri  Mpina.

Hivyo Serikali inawaomba wadau wote walioathirika kwa namna moja au nyingine na uendeshaji wa machinjio hiyo waipe muda Serikali kushughulikia changamoto zilizopo na kwamba katika kipindi cha muda mfupi Machinjio ya Dodoma itafufuliwa na kupanuliwa kuwa ya kisasa zaidi.

Waziri Mpina kwa muda mrefu Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kurekebisha kasoro za uendeshaji wa Machinjio ya Dodoma kama sharti muhimu katika Mkataba wa Mauzo ya Mali kwenye Ibara ya 4.1.3.1 na kwa kuwa jitihada za kuinusuru Machinjio hiyo zimefanyika kwa muda mrefu bila ya mafanikio yoyote.
Hivyo Serikali imejiridhisha kwamb Mbia (NICOL) amekiuka vipengele muhimu vya Mkataba katika Ibara ya 7, 13, 6, 9 na 102; Pia NICOL imekuwa ikifanya biashara na mali za Kampuni bila ya kuwekeza na bila ya kutoa gawio kwa Serikali kwa kipindi chote cha miaka 11 alichokabidhiwa Kiwanda hicho;
Waziri Mpina amesema tangu machinjio hiyo ibinafsishwe Serikali imeendelea kupata hasara na mali nyingi za Kampuni kama mitambo, majengo, magari na rasilimali nyingine zimechakaa na hakuna ukarabati wowote uliofanyika;
Pia nchi yetu imepoteza ajira, fedha za kigeni, biashara na masoko ya mazao ya mifugo baada ya Kiwanda kufungiwa kuuza mazao ya mifugo katika nchi za Jumuiya ya Kiarabu (UAE).
Aidha, Kampuni 10 zilisimama kusafirisha na kufanya biashara ya nyama baada ya Kiwanda kufungiwa ambapo kwa mwezi mauzo ya nyama nje ya nchi katika Machinjio yalikuwa yamefikia tani 192 sawa na mbuzi 24,000 kwa mwezi. Pia, kiwango cha uchinjaji wa ng’ombe kushuka kutoka wastani wa ng’ombe 120 hadi 50 kwa siku;
Pia Hasara na madeni ya Kiwanda cha TMCL yanaendelea kukua kila uchao huku Mbia (NICOL) akishindwa kurekebisha kasoro zilizobainika katika vipindi tofauti hata baada ya kupewa notisi ya muda wa siku 30 na hata Mbia mwenzake (NARCO) kumpa notisi ya siku 180, pia, ziara za Viongozi katika Machinjio akiwemo Waziri wa Mifugo na Uvuvi;
Waziri Mpina amesema Mbia (NICOL) amekiri kukosa uwezo wa kimtaji na utaalam wa kuendesha machinjio hayo kupitia kikao cha tarehe 27/12/2019 cha Wadau wote wakiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, NICOL, NARCO, TMCL, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma na Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambacho alikiitisha
 kufanya tathmini ya utekelezaji wa marekebisho ya kasoro baada ya notisi ya siku 30 kuisha tangu tarehe 08/12/2019.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.