Barua kwa mh Rais.
Miaka 60 iliyopita siku kama ya leo huko ardhi ilikuwa imetulia tuli huku miti ikichezacheza na kuzalisha hewa nzuri ya oksijeni. Ikasikika sauti za ndege na wanyama zikitoa nyimbo nzuri nzuri zilizonakshiwa zenye kuashiria jambo la kihistoria katika nchi hii.
Wahenga wenye kun'gamua mambo wakapata ishara kuwa hii jambo halitokei aghalabu kutakuwa kuna jambo. Basi ndio mama mmoja kutoka huko chato akapata kujifungua mtoto ambaye leo hii amekuwa mkombozi wa watanzania pamoja na kuwa mfano mzuri wa nchi nyingine juu ya ufanisi wake wa kazi. Anaitwa Magufuli ila sisi tunamuita bulldozer, chuma , jiwe na kimbilio la watanzania ambao walikuwa walishakosa matumaini na nchi yao.
Mlimwengu mimi leo nimeamka na kidumu changu cha maji cha lita tano nipate kuelekea ikulu kusherehekea siku yako ya kuzaliwa na kukumwagia maji ikiwa ni ishara ya salamu kutoka mtaani kwetu maana ilikuwa ni miaka mingi watu wa Kibangu na Riverside hawana maji ila sasahivi maji ni kuanzia asubuhi mpaka jioni. Hivyo maji hayo yangeashiria kazi kubwa ambayo umeifanya kuhakikisha wananchi wako wanapata maji na unajua kuwa maji ni uhai.
Ila nimezuiliwa na wazee kuwa siko serious ila hayo maji nitajimwagia mwenyewe kuridhisha moyo wangu.
Huku kwetu tuna msemo usemao kuwa ' Enkobe ekanyampira eibale norwo olatagamba wakahurila' kwamba nyani alijambia jiwe na kusema kuwa hata kama hujasema chochote ila habari imeipata.
Point yangu ni kuwa kazi unayofanya wanaona ni kwamba wana macho ila wanajifanya wametia viboriti machoni wana masikio wanajifanya wameweka pamba ili wasisikie.
Hii ni habari njema ambayo watanzania walikuwa wanaitaka na wapingaji hawajahi kukosekana. Hata mitume wa Mungu walipingwa na wengine wakauliwa sembuse hawa wachumia tumbo.
Vaa mkanda vaa buti wananchi tumeelewa mlimwengu mimi huwa nakaa na walimwengu na hao ndio wanaoiona kazi unayoifanya. Hizi kelele za chura hazina maana haziwezi kuzuia watu tusinywe maji.
Kazi hii unayopiga ni kubwa sana imefikia hatua hadi wananchi wanaona kipindi ulichopewa ni kidogo unahitaji kupata muda mrefu ila hawajui kuwa katiba ndio inayokuweka labda mpaka pale itakaporekebishwa.
Mambo unayoyafanya siyo hadithi za abunwasi kama ni miundombinu imeonekana, sasa hivi tunapokea madege ambayo tulikuwa tunayaona kwenye mataifa ya wenzetu. Miradi mikubwa ya reli pamoja na barabara zinazojengwa kwa ufanisi wa hali ya juu.
Nichukue nafasi hii utusamehe baadhi ya watu tunalalamika kuwa unaleta maendeleo ua vitu badala ya watu. Ila hawajui kuwa hayo ya vitu ndio yatakayopelekea kupata ya watu. Miundombinu unayoijenga taifa litakukumbuka maana kazi zitakuwa zimerahisishwa sana.
Ni mtu pekee ambaye umetujengea imani ya kutupa nguvu kwamba Tanzania inaweza kuwa nchi kubwa tukajitegemea pasipo kutegemea misaada kutoka nje na kweli matunda tunayaona sasahivi unatuletea madreamliner kwa uchumi wetu wa ndani.
Hii ni imani kubwa ambayo umetujenga sasahivi vijana wengi wanawaza kuwa na viwanda vyao kwa sababu ya imani uliyotupa kuwa tanzania ya viwanda inawezekana.
Mchawi mpe sifa zake na msema ukweli ni mpenzi wa mwenyezimungu viatu ulivyovivaa ni size yako wengine viliwapwelepweta ila leo hii vibaka wote umewabana, watu walikuwa wananeemeka peke yao huku wavuja jasho wanaumia. Ila sasahivi utakula chakula ulipopeleka mboga.
Una mengi umeyafanya siwezi kuyamaliza hapa ili nikutakie kheri katika siku yako ya kuzaliwa na kazi njema katika ujenzi wa nchi hii.
Wako
Mlimwengumimi
Mohamed Ismail
0762 07 03 61
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.