Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Mkuu Dk. Ferdinand Shoo amewaonya viongozi wa Tanzania na kuwataka watumie nafasi zao kuwasaidia wengine hasa wale wenye uhitaji.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akitoa mahubiri kwenye ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP, Dkt. Reginald Mengi iliyofanyika kwenye kanisa la KKKT, Usharika wa Moshi mjini.
Amesema kuna watu wakipata vyeo ama utajiri kidogo tu, wanatumia nafasi zao kunyanyasa wengine na akaonya Watanzania wasie wepesi wa kuhukumu, kunyanyasa wengine au kubagua wengine.
Katika mahubiri yake, Dk. Shoo amesema kama kuna dhambi ambayo binadamu anapaswa kuifanyia toba ni ile ya kubaguana na kama Watanzania wanahitaji Taifa lipokee baraka kutoka kwa Mungu, ni vema wakaacha kufanya hivyo. Amesema dhambi nyingine inayopaswa kufanyiwa toba ni ile ya watu wenye nafasi kuwakanyaga wengine.
“Ndugu zangu tukiwa na cheo, tukiwa matajiri, tukiwa na uwezo tuvitumie kuwasaidia wengine, tuache ubinafsi, tuache kiburi, tuache kujitutumua hasa kwa viongozi wa umri mdogomdogo. Kuna mahali mmefika mnajitutumua kama chatu, acheni kabisa. Naomba tuwe unyenyekevu ndugu zangu.”
Ameendelea kwa kusema, “Wale wanaopata utajiri, acheni kukumbatia mali zenu, toeni na kuwasaidia wenye uhitaji kwani mnapata satisfaction kwa kufanya hivyo. Huu ni ujumbe kwetu sote na Mungu atusaidie tulishike hili. Muendelee kuiombea familia na yale mazuri mengi tuliyojifunza kwake tukayatende tukayatende, tuyaenzi,” amesema.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.