Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amesema sekta ya afya ni nyeti isiyopaswa kuingiliwa na Wanasiasa ila Madaktari na wauguzi wanapaswa kutimiza wajibu wao ipasavyo ikiwemo kuzuia vifo vya mama na mtoto.
Mnyeti aliyasema hayo mjini Babati, wakati akizungumza na wakuu wa wilaya, wakurugenzi, madaktari na wauguzi kwenye uzinduzi wa kampeni ya jiongeze tuwavushe salama.
Alisema kazi ya viongozi ni kusimamia utekelezaji na madaktari na wauguzi wafanye kazi zao kwa vitendo huku wakitumia lugha nzuri pindi wanapotoa huduma kwa wagonjwa.
Alisema wataalamu wa afya wanapaswa kutimiza wajibu wao katika uwajibikaji na kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga waweze kuwa watu wazima.
“Kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anatimiza jukumu lake ikiwemo kupatiwa huduma bora ili kudhibiti vifo vya kina mama na watoto pamoja na kutoa elimu kuanzia ngazi ya jamii,” alisema Mnyeti.
Alisema kwa mujibu wa sera za afya nchini, huduma za uzazi hutolewa bure ila kuna baadhi ya maeneo malalamiko ya mama wajawazito kudaiwa fedha yamekuwa yakitolewa.
“Halmashauri na wengineo kasimamieni hilo inawezekana suala la kuwatoza fedha wajawazito au wa mama waliojifungua halipo kwetu ila lichunguzwe na kufanyiwa kazi,” alisema Mnyeti.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.