ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, November 13, 2018

RC SONGWE ATOA SULUHU MGOGORO WA UCHIMBAJI MADINI

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus E. Mwangela akikagua shughuli za wachimbaji wadogo wa madini Wilayani Songwe ambapo ameagiza Ofisi ya Madini kuwatembelea wachimbaji na kuwapa elimu kuhusu sheria na taratibu za uchimbaji wa madini.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus E. Mwangela akiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wamesuluhisha mgogoro baina ya wakazi wawili wa kijiji cha Saza Wilaya ya Songwe kuhusu eneo la uchimbaji wa madini.
Brig. Jen. Mwangela amesema Suzan Karan amebainika kisheria kuwa ni mmiliki halali wa eneo lililokuwa likigombewa kwa kuwa ana leseni halali huku Elimbotwa Naftari ambaye hana leseni na amekuwa akidai umiliki wa eneo hilo amebainika kuendesha shughuli za uchimbali kinyume na sheria.
“Sheria inamtambua Suzan kama mmliki halaki kwakuwa anayo leseni na amefuata taratibu na sheria za uchimbaji madini, tunashauri Elimbotwa kama atataka kuendelea kuchimba madini katika eneo hilo basi akubaliane na Suzan kufanya naye kazi”, amesisitiza.
Ameongeza kuwa serikali za vijiji hazina mamlaka ya kuwapa vibali vya uchimbaji wawekezaji wa madini bali leseni na vibali vyote vya uchimbaji wa madini hutolewa na ofisi za madini Wilaya, mkoa au kanda, hii inatokana na kuwa serikali ya kijiji ilimtambua Elimbotwa kama mmiliki wa eneo la uchimbaji kinyume na sheria.
Kwa upande wake Elimbotwa amesema anamtambua Suzan kama mmliki halali wa eneo walilokuwa wakiligombania isipokuwa sasa anadai fidia ya zaidi ya shilingi milioni 190 ikiwa ni gharama ya vitu alivyowekeza kabla ya Suzan kupewa leseni ya eneo hilo.
Naye Suzan ameupongeza uongozi wa Mkoa kwa kutoa suluhu ya mgogoro huo kutokana na kuwa ulipelekea kusimama kwa shughuli za uchimbaji na hivyo kuathiri uchumi wake.
Aidha Brig. Jen. Mwangela ameagiza Takukuru, TRA na taasisi zinazoweza kufanya ukaguzi, zihakiki madai ya Elimbotwa kama ni halisi ili Suzan aweze kuyalipa.
Imeelezwa kuwa baadhi ya migogoro ya haki ya kumiliki maeneo ya uchimbaji wa madini mkoani Songwe inasababishwa na ukiukwaji wa taratibu na sheria za madini unaofanywa na baadhi ya watendaji na wachimbaji.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.