Na John Walter-Babati
Halmashauri ya mji wa Babati imeanza zoezi la kuwaondoa Wafanyabiashara wadogo wadogo [Machinga] wanaofanya shughuli zao kwenye maeneo yasiyo rasmi.
Hata hivyo baadhi yao waliozungumza na Muungwana Blog, wamesema kuwa wanafanyia biashara nje ya maeneo rasmi yaliyotengwa kwa biashara kwa sababu ya ukosefu wa wateja hali inayowalazimu kutembeza kuwatafuta mitaani.
Wafanyabiashara hao wamesema baada ya kufukuzwa hawajui waelekee wapi huku wakiomba serikali ya Rais John Magufuli iwasaidie kwani wanadaiwa pesa za mikopo na ndio tegemezi kwenye familia zao.
Baada ya malalamiko ya wafanyabiashara hao kituo hiki kikazungumza na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Babati Fortunatus Fwema ambaye amesema wameamua kuwaondoa wafanyabiashara hao baada ya kukiuka agizo lililotolewa muda mrefu kuhamia katika maeneo yaliyotengwa.
Amesema kwamba wanatekeleza agizo la serikali la kuwatafutia wafanyabiashara maeneo ya biashara lakini cha kushangaza hawataki kuyatumia na badala yake wanapanga bidhaa zao kwenye maeneo ambayo hayajaidhinishwa.
“Ni wajibu wetu kama halmashauri kuhakikisha mji unapangika na katika kutekeleza hilo lazima tuwatafutie wafanyabiashara wanaouza mboga mboga na wengine maeneo maalum ya kufanyia shughuli hizo,na kwa kuzingatia hilo tumejenga soko darajani na Silent Inn ambalo limezinduliwa na mbio za mwenge mwaka jana” alisema Fwema.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.