ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, September 7, 2018

KANUNI 10 ZAPITISHWA KUMLINDA MTOTO.

 Kamati ya maendeleo ya kata ya Igogo Nyamagana,  Mwanza  kwa kushirikiana na Shirika la wotesawa sept 6, 2018 walipitisha kanuni kumi(10) za kumlinda mtoto mfanyakazi wa nyumbani kwa lengo la kuondoa migogoro na migongano iliyopo kwenye mitaa yao kwa ajili ya wafanyakazi wa majumbani.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mwenge kata ya Igogo wilayani Nyamagana Ramadhan Salum Mahira ambaye ni mwenyekiti wa kikao kazi hicho alisema wamefikia maamuzi hayo kutokana na vitendo mbalimbali vya ukatili dhidi ya watoto wafanyakazi vinavyoendelea kufanyika katika kata hiyo.

“Kata ya Igogo ni moja kati ya kata zenye migogoro mingi baina ya waajiri na watoto wafanyakazi za nyumbani hivyo wenzetu wote sawa walipokuja tukaona kuna haja ya kuandaa hizi kanuni kwa lengo la kuondoa hiyo migogoro na migongano na kweli tumefanikiwa na leo hii ndiyo tunazipitisha ili ziende kutumika ambazo tunaamini zitaleta usawa”alisema Menyekiti Ramadhan 

Aidha amesema kanuni hizo zitaleta muelekeo pamoja na kupunguza migongano na migogoro kwa jamii na  wengine watajifunza kutoka katika kata hiyo kwa sababu kila mtu atajua haki na wajibu wake kwa mwingine.

Nao wenyeviti wa mitaa mbalimbali iliyopo kwenye kata hiyo walielezea kufurahishwa na kanuni hizo wakisema kutokuwepo kwake ni chanzo cha matatizo kwenye mitaa wanayoiongoza huku wakikiri kuwa hawakuwahi kuwa na kanuni hizo.

Wamezitaja faida mbalimbali watakazonufaika nazo watoto wafanyakazi za nyumbani kuwa ni jamii kutambua haki zao zikiwemo haki ya kupata likizo, kulipwa mshahara wake kwa wakati, haki ya kupatiwa huduma za matibabu pamoja na  kiwango cha mshahara.

“tulikuwa hatuna hizi kanuni kwahiyo zitatusaidia sana katika kusaidia wafanyakazi kwenye majumba wafanyakazi watakuwa wamepata faida kubwa kwani wengi wao pia walikuwa hawazijui wala kuzitambua  kwahiyo zitawasaida sana”

“kwa upande wetu wenyeviti  ilikuwa yakitokea matatizo hatujui wapi tuanzie ila kupitia kanuni hizi tumepata utaratibu wa kuanzia”alisema Anthony Kimazi M/kiti wa mtaa wa Kambarage

Kwa upande wake muwakilishi wa shirika la wote sawa ambalo ndilo muandaaji wa kikao kazi hicho Elisha David amesema shirika lipo katika utekelezaji wa mradi wa ushirikishwaji wa wafanyakazi za majumbani ambao umefanyika katika kata 6 zilizopo Nyamagana.

Amesema kanuni hizo ni matokeo ya vikao baina yao na kamati za maendeleo ya kata WODC ambapo kupitia vikao hivyo waliamua kuandaa kanuni ambazo lengo lake ni kuleta ushirikiano kati ya pande hizo na zitaondoa migogoro mingi pamoja na changamoto zinazojitokeza.

“lengo ni kuboresha uhusiano tukiamini kuwa mfanyakazi ana thamani kubwa kwenye familia, kwani mwajiri akiondoka kazini anamwachia binti nyumba yenye thamani kubwa na vitu vingi ndani yake, kama hakuna mahusiano mazuri wanaweza kufanya vitu vibaya sana”Alisema Elisha

Miongoni mwa kanuni hizo kumi(10) zilizoandaliwa ambazo zitatumika kwenye mitaa yao ni pamoja na kila muajiri anatakiwa kumsajili mfanyakazi wa nyumbani katika uongozi wa serikali ya mtaa, kila mtaa uandae orodha ya wafanyakazi wa nyumbani, mwajiri atoe mkataba na mwajiri kutoruhusiwa kuajili mtoto chini ya miaka 13, Mwajiri kutomuajiri mtoto mwenye umri chini ya miaka 14  na nyingine inasema mfanyakazi wa nyumbani atamtii na kumuheshimu mwajiri wake.




Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.