ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, July 9, 2018

ALIYEANDAA SHOW YA WERRASON MWANZA ALA ZA USO MBAYA



MUANDAAJI wa tamasha la Mwanamuziki maarufu barani Afrika, Werrason Ngiama Makanda, anayekwenda kwa jina 'HAPA KAZI PROMOTERS' amekula za uso baada ya mashabiki kuingia mitini katika show yake hiyo.

Kwa mujibu wa Gazeli la Mwanaspoti, Mwandaaji huyo wa Shoo ya Werrason, Lengos VIP amesema kuwa amechukizwa na mashabiki wa Mkoa wa Mwanza kutojitokeza kwa wingi na kuapa hatarudia kupeleka wasanii mkoani humo.

Alisema kuwa alimgharamia Werrason na aliamini watapata watu ukumbini, lakini ilikuwa tofauti na matarajio yake hivyo naye kuamua kuondoka ukumbini.

“Sitarudia, nasema hivi sitarudia tena kuleta msaniii yeyote Mwanza. Nilitumia gharama kubwa takribani 30 milioni, lakini hata 2 milioni sikuiona” amesema VIP na kuongeza.

Lengos alisema, “Nilimwambia hata yeye ‘Werrason’ kwamba aachane na shughuli unajua wale wasanii wakubwa wanafanya kazi kwa kuona watu wametosha ukumbini, tofauti na hapo ni bure,” amesema.

Rais huyo wa Wakongo nchini, amebainisha kuwa amebaini sababu ya kutoitikia kwa mashabiki na kusababisha changamoto kwa msanii wake kufanya au kutokufanya shoo ni kutokana na kukosa matangazo.

MTAANI WADAU WANASEMAJE?
Mashabiki wa burudani wamemponda muandaaji huyo na kamati yake kutumia mbinu za kizamani katika kufanya promosheni ya show hiyo kiasi cha ujumbe kushindwa kuwafikia wananchi kwa mashiko yanayotakikana.
"Mimi mwenyewe nilizipata habari za ujio wa huu saa chache kabla ya kuanza show, ilikuwa mida ya jioni hivi na ni kupita instagram, naperuzi tu kutizama mambo yangu nikaona picha, nikaona nisome, jeh ningeibukaje kwa uchumi huu? Huwezi kukurupuka. Hata akija msanii mkubwa wa Marekani kama Chriss Brown bila matangazo ya kutosha, anakula za uso" alisema mdau wa burudani Shija Kazinja mkazi wa Mecco jijini Mwanza.
"Muandaaji amemkosea sana Werrason, kashusha hadhi yake na kuonekana kama hakubaliki wala hafahamiki, nilifikiri ni wasanii wenyewe ndiyo hujiporomosha kwa kufanya kazi mbaya kumbe laa hata waandaaji nao wanamchango katika kuporomosha hadhi za wasanii, hii itamwogopesha sana Werrason kuhusu Tanzania" alisema Zephania Bundala mkazi wa Nyamagana jijini Mwanza.

Licha ya kuwa na stage kubwa na sound ya maana katika ukumbi wenye uwezo wa kuingiza watu elfu nne, eneo lilikuwa na watu wasiozidi thelathini kiasi cha kumsababisha Werrason kushindwa kupanda jukwaani kutumbuiza zaidi ya kujitambulisha na kisha kufungua fursa ya kupiga picha na mashabiki kiduchu waliofika ukumbini hapo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.