ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, April 5, 2018

RAIS MAGUFULI ASIKITISHWA NA AJALI YA TABORA.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ajali iliyotokea usiku wa jana Mkoani Tabora na kusababisha vifo vya takribani watu 12.

Dkt. Magufuli ameeleza hayo kwenye salamu zake za rambirambi alizozitoa leo Aprili 05, 2018 baada ya kupita siku moja tokea basi la kampuni ya City Boy lililokuwa limebeba abiria kutoka Karagwe Mkoani Kagera kuelekea Dar es Salaam kugongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso lililokuwa linatoka Singida kuelekea Igunga.

“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu 12 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea jana usiku katika wilaya ya Igunga mkoani Tabora, nawapa pole wafiwa wote, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu mkubwa. Nalitaka Jeshi la Polisi, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na Mamlaka zote zinazohusika na usalama wa barabarani kujitathmini, na kutafuta majawabu ya kwa nini ajali za barabarani zinaendelea kutokea kwa kusababishwa na uzembe na uvunjaji wa sheria za barabarani?”, amesema Dkt. Magufuli.

Pamoja na kutoa pole kwa wafiwa, Dkt. Magufuli amewataka viongozi wote wanaohusika na usimamizi wa usalama wa barabarani kutafakari kwa nini ajali nyingi zimekuwa zikitokea katika maeneo yaleyale na kutafuta ufumbuzi ili kuepusha madhara ya watu kupoteza maisha, kupata ulemavu wa kudumu na kupoteza mali.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.