ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, March 12, 2018

NKURUNZINZA ATANGAZWA KUWA KIONGOZI WA MAISHA WA CHAMA CHA CNDD-FDD

 Nkurunzinza atangazwa kuwa kiongozi wa maisha wa chama cha CNDD-FDD

Chama tawala nchini Burundi cha CNDD/FDD kimemtangaza Rais Pierre Nkurunzinza wa nchi hiyo kama kiongozi mkuu wa kudumu au kiongozi wa milele ndani ya chama hicho.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya vikao vya siku tatu vya mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika katika eneo la Buye anakozaliwa Bwana Nkurunziza kaskazini mwa nchi hiyo.
Chama tawala cha CNDD-FDD kimechukua uamuzi huo  wakati Burundi inajiandaa kufanya marekebisho ya Katiba ili kumruhusu Rais Nkurunziza kuendelelea kuongoza taifa hilo hadi mwaka 2034.
Taaarifa fupi ya chama cha CNDD/FDD imesema kuwa, vikao hivyo vilikusudia kuimarisha chama tawala na taasisi zake.
Lakini pia chama hicho tawala kimechukua uamuzi wa kumuongezea hadhi na kumpa cheo cha juu Rais Nkurunziza na hivyo kumtangaza kuwa ni kiongozi mkuu wa kudumu ndani ya chama.

Vikosi vya usalama Burundi vimekuwa vikituhumiwa kwa kukiuka haki za binadamu

Tangazo hili la chama tawala CNDD-FDD la kumfanya Rais Nkurunziza kama Kiongozi Mkuu wa Kudumu linajiri wakati Burundi inajiandaa kwa kura ya maoni kuhusu marekebisho ya Katiba baadae mwezi Mei. 
Wadadisi wengi wa siasa za Burundi wanaamini kuwa, hatua hii ya chama tawala inanuwia kumalizia mapema mjadala wa mtetezi wa kiti cha Urais kwa niaba ya chama hicho na kuonyesha mustakabali wa uongozi kabla hata uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2020.
Burundi ilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mara ya tatu mfululizo. Asasi mbalimbali za kieneo na kimataifa zimeendelea kuituhumu serikali ya Burundi kwamba, inakiuka haki za binadamu tuhuma ambazo zimekuwa zikikanushwa na serikali ya Bujumbura.

CHANZO:- http://parstoday.com/sw/news/africa

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.