Na Mwandishi Wetu
Mfanyabiashara na mmiliki wa mabasi ya Super Sami, Samson Josiah maarufu Super Sami, atazikwa leo Alhamisi Machi 16, nyumbani kwao wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza saa tisa alasiri baada ya uchunguzi wa kitatibu kukamilika.
Kaka wa marehemu Amini Sambo amesema atazikwa leo Magu Mjini baada ya kusafirishwa kutoka Musoma ambako mwili wake ulipelekwa kwa ajili ya uchunguzi.
Mfanyabishara huyo anadaiwa kutoweka Februari 27, mwaka huu nyumbani kwake eneo la Mwananchi-Buzuruga Kata ya Mahina Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza na gari lake kupatikana Machi 9, mwaka huu likiwa limeteketea kwa moto kando ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kisha mwili wake kupatikana Machi 14, mwaka huu ukiwa umefungwa kwenye viroba ndani ya Mto Rubana.
Ilielezwa kuwa siku aliyotoweka Super Sami alikuwa katika harakati za ununuzi wa nyumba katika Mji Mdogo wa Ramadi Wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu eneo ambalo ni njia kuu ya kwenda mkoani Mara na jirani na lango la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mpaka sasa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limetangaza kuwashikilia watu watano ambao majina yao hayajatajwa kwa uchunguzi wa kifo cha Super Sami, huku habari za ndani ya zikieleza kuwa wanaoshikiliwa ni pamoja na watu waliohusika na kuwasiliana naye siku ya tukio ikiwa ni pamoja na kutaka kuuziana naye nyumba hiyo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.