ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, November 12, 2017

NYALANDU ASHINDWA KUPANDA JUKWAANI MKUTANO WA CHADEMA.

Aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu aliyejiondoa CCM siku 12 zilizopita ameshindwa kupanda jukwaani mjini Mtwara katika mkutano wa Chadema.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana Jumamosi Novemba 11,2017 akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Saranga jijini Dar es Salaam alisema amempokea Nyalandu na leo Jumapili Novemba 12,2017 angeungana naye kwenye mkutano wa kampeni mjini Mtwara.

Hata hivyo, kukosekana kwa ndege inayofanya safari kati ya Dar es Salaam na Mtwara kumemsababishia Nyalandu kushindwa kuhudhuria mkutano huo.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema Nyalandu aliyekuwa Nairobi nchini Kenya kumjulia hali Tundu Lissu amekosa ndege ya kwenda Mtwara.

Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki anaendelea na matibabu ya majeraha ya risasi katika Hospitali ya Nairobi, Kenya. Alishambuliwa akiwa maeneo ya makazi yake Area D mjini Dodoma Septemba 7,2017.

Mrema amesema Nyalandu amefika Dar es Salaam lakini kwa bahati mbaya hakuna ratiba ya ndege ya Mtwara kwa leo Jumapili Novemba 12,2017.

"Tunaomba radhi, tukio hilo tunaliandalia mahali pengine na wakati ukifika tutakuwa pamoja naye," amesema Mrema.

Nyalandu baada ya kujiondoa CCM, aliiomba Chadema imfungulie “malango”.

Alipomtembelea Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema ofisini kwake Mikocheni, Dar es Salaam hivi karibuni, Nyalandu alimshukuru “kwa kuonyesha njia kwa wengine kuwa kuna maisha nje ya CCM”.

Viongozi wa juu wa Chadema wamejipanga kuongoza kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 nchini.

Chama hicho kimeunda kamati za kitaifa 10 zitakazokwenda kuongeza nguvu, hamasa na mikakati ya kampeni za uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 26.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.