Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba Haji Manara.
LICHA ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumfungia kiungo wa Mbao FC, Pius Buswita, kutocheza soka kwa kipindi cha mwaka mmoja kutokana na kusaini kuzichezea klabu mbili tofauti, Simba na Yanga, sasa ataburuzwa mahakamani, imeelezwa.
Klabu ya soka ya Simba, imesema inatarajia kumfikisha mahakamani Buswita, kwa madai kuwa amewatapeli fedha zao wakati akijua alishasajiliwa na Yanga.
Hata hivyo, Simba haikuwa tayari kuweka wazi kiasi cha fedha ambacho mchezaji huyo alichukua wakati anasaini mkataba kwa ajili ya kuwatumikia mabingwa hao wa Kombe la Shirikisho.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema klabu yake imefikia hatua hiyo kutokana na lugha za kejeli ambazo zimekuwa zinatolewa na nyota huyo na baadhi ya wadau hali ya kuwa klabu yake ilikosewa kwenye usajili huo.
Manara alisema Simba inataka vyombo husika kumchukulia hatua za kisheria mchezaji huyo wa zamani wa Mbao FC ya jijini Mwanza na lengo lake ni kumfanya kuwa fundisho kwa wachezaji ambao wanania ya kufanya kosa la aina hiyo.
"Haikuwa nia yetu kuchukua hatua hii, tulidhani ilikuwa ni nafasi ya sisi na wenzetu wa Yanga kukaa na kukubaliana ni timu ipi anataka kuichezea ili kunusuru kipaji chake, huku tukiamini mchezaji atakaa na kujutia kosa lake, lakini tumeumizwa na lugha chafu na kejeli ambazo zinatumiwa na wenzetu wa Yanga kuwatisha viongozi wa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania)," alisema Manara.
Aliitaka TFF kuendelea kutenda haki kama ilivyofanya kwa Buswita na kusisitiza kwamba Simba haitaki kupendelewa na inasisitiza haki iendelee kutolewa kwa wachezaji wengine kama ilivyofanya kwa kiungo huyo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.