ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, July 29, 2017

CCM ARUSHA YAPATA PIGO.

KATIBU wa Uchumi na Fedha wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Mkoa wa Arusha, Hillal Soud amefariki dunia jana nyumbani kwake Njiro majira ya saa tatu usiku.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho mtoto wa marehemu Ramadhan Soud alisema marehemu baba yake alikuwa anasumbuliwa na shinikizo la damu.

Alisema kabla ya marehemu baba yake kufikwa na umauti alipatiwa matibabu katika hosptali ya Shirhindu ambapo afya yake iliimarika na kurudishwa nyumbani.

Akizungumzia kifo cha Soud kwa niaba ya CCM Mkoa wa Arusha Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Shaaban Mdoe alisema chama kimepokea msiba huo kwa mshtuko mkubwa kwani juzi walikuwa naye kwenye kikao cha Sekretararieti ya mkoa.

Kwa mujibu wa Mdoe Julai 26 mwaka huu walikuwa na marehemu kwenye kikao akiwa mzima wa afya, lakini baada ya muda aliwaambia kuwa anasikia maumivu ya kichomi chini ya kifua mkono wa kushoto.

“Naisikia sauti ya marehemu kwenye masikio tangu hapo mpaka sasa baada ya kusema anasikia kichomi alitania wajumbe wa kikao nitakufa nini nina miaka 62, kisha kanigeukia na kuniambia nyie ni vijana mna nguvu ya kukimbia kimbia na kukipigania chama,”alisema.

Alisema hata hivyo aliendelea na kikao hadi kilipomalizika jioni bila tatizo lolote ambapo aliagana na wajumbe na kuelekea nyumbani kwake.

Alisema siku iliyofuata kulikuwa na kikao cha kamati ya siasa ya mkoa ambapo alimtumia ujumbe wa meseji Katibu Msaidizi wa CCM mkoa  Omary Bilal kumjulisha kuwa hajisikii vizuri hivyo hataweza kushiriki kikao na kwamba amepumzishwa kwa muda katika hosptali ya Shir Hindu iliyopo mkoani hapa.
Mdoe aliendelea kufafanua kuwa baadaye jioni majira ya saa 10  hivi alimtumia tena ujumbe katibu huyo na kumjulisha kuwa afya yake imeimarika na kwamba ameruhisiwa kwenda nyumbani.

“Baada ya kupata taarifa hiyo katibu wa CCM  mkoa Elias Mpanda  alimpigia simu kumjulia hali ambapo alijibu kuwa anandelea vizuri na ameruhusuwa kwenda nyumbani kupumzika,”alisema
Kwa mujibu wa mdoe usiku majira ya saa tatu alipata taarifa kuwa marehemu alianguka ghafla nyumbani kwake na kufikwa na mauti.

Alisema CCM imepata pigo kwa kupoteza kiungo muhimu ambaye alikuwa amebobea katika masuala ya fedha na utawala ambapo alikisadia chama katika masuala mbalimbali ya kukuza uchumi wa chama pamoja na jumiya zake.

“Tumepata pigo kubwa Soud alikuwa kwenye mchakato wa kupata wawekezaji wa kuwekeza kwenye maeneo yetu ya wazi Sakina na Njiro lakini pia kuboresha uwanja wa Sheik Amir Abeid, lakini pia alitusaidia  kurekebisha bajeti ya uchaguzi wa jumuiya za chama,”alisema

Kabla ya kuwa mchumi wa CCM mkoa wa Arusha Soud alikuwa Mkurugenzi wa NMB Kanda ya Kaskazini,mpaka alipostaafu.

Marehemu Soud ameacha  watoto sita na mjane mmoja na  amezikwa leo(jana) katika makaburi ya njiro .

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.