Taarifa zilizosambaa kupitia mitandao ya kijamii zimeeleza kuwa akaunti zote za kampuni hiyo zimefungiwa mpaka pale watakapolipa deni hilo, lakini kampuni hiyo imetoa ufafanuzi.
Ujumbe huo uliongeza kuwa kampuni hiyo imefikishwa mahakamani na benki moja hapa nchini kwa madai ya kutaka kulipwa Sh600 milioni, baada ya kuingia makubaliano ya kulipa wafanyakazi wake mishahara pamoja na mikopo lakini mpaka sasa imeshindwa kurejesha fedha hizo.
Hata hivyo, akizungumzia suala hilo mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya Sahara, Anthony Diallo alikiri mamlaka hiyo kufungia akaunti ya kampuni yake.
Diallo ambaye ndiye mmiliki wa kampuni hiyo alisema ni akaunti moja tu iliyofungiwa na kwamba anaamini baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na mamlaka hiyo watafikia muafaka ili biashara ziendelee kama kawaida.
“Tutalimaliza hakuna kitakachoenda mrama,” alisisitiza Diallo ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, pia aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo nafasi ya Waziri wa Maliasili na Utalii na Naibu Waziri wa Maji, Maendeleo ya Mifugo katika Awamu ya Nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Amesema deni la TRA linatokana na kodi iliyopatikana baada ya ukaguzi wa vitabu kwa miaka mitatu.
“Ni ukaguzi wa kawaida hufanyika kama taratibu. Sasa kwa sababu ya kuhamisha matangazo yetu kutoka analojia kwenda digitali ilibidi tukope benki, ujenzi na kumaliza mradi imechukua miaka mitatu. Wakati wote tumekuwa tukilipa riba benki na zinazobaki toka mauzo ya matangazo tunalipa mishahara, umeme na malipo ya kodi za kawaida,”alisema.
“Ni kawaida ila wamefanya hatua za kutuaibisha tu. Kampuni yetu ya ving’amuzi ni ya Kitanzania na mapato yote yanaingia nchini wakati kampuni nyingine kubwa zote ni za kigeni kutoka China, Afrika Kusini, Mauritius na Kenya! Ukweli sisi tunahitaji kusaidia nchi kiuchumi na kutuharibia ni hasara kwa nchi.”
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.