NA ANNASTAZIA MAGINGA,Mwanza
MAHAKAMA kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza imetupilia mbali pingamizi la shauri dogo kwenye kesi ya msingi ya mauaji ya aliyekuwa kamanda wa polisi mkoa wa mwanza, Liberatus Barlow, lililokuwa likipinga kupokelewa kwa kielelezo namba 24 cha maelezo ya onyo kama ushahidi mahakamani hapo.
Pingamizi hilo liliwasilishwa jana na wakili wa mshitakiwa wa sita, Maduhu Ngassa baada ya shahidi wa 16 Vedastus Pius ambapo upande wa mashitaka uliomba kupokelewa kwa kielelezo hicho kama ushahidi.
Pingamizi hilo lilikuwa limejikita katika hoja mbili ambapo upande wa mshitakiwa ulidai kulikuwa na ukiukwaji wa sheria ya mashitaka kwa sababu maelezo yaliyotolewa siyo ya mshitakiwa hivyo sheria haikuzingatiwa na kulikuwa na ukiukwaji wa sheria ya ushahidi kwa sababu mshitakiwa hakupewa nafasi ya kufanya masahihisho kwenye maelezo yake na kwamba ilitumika nguvu.
Akitoa maamuzi ya pingamizi hilo, Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Sirilius Matupa, amesema kifungu kilichotumika na upande wa utetezi hakiusiki na utoaji wa maelezo bali kinahusika wakati wa ukamataji ambapo hutoa haki ya mtu anayekamatwa na kwamba kifungu sahihi kinavchohusika na utoaji maelezo ni cha 50 (2) b (1) kinachomruhusu muandika maelezo kumpa fursa anayehojiwa kuita mtu atakayeshuhudia wakati wa utoaji maelezo.
“Sijaridhika na ushahidi uliotolewa kwamba kulikuwa na mazingira ya kutumia nguvu katika kutoa maelezo ingeonekana tofauti kama hakusomewa maelezo yake au kulikuwa na ubishi.
“Baada ya kupitia hoja zote na kwa ajili ya kutoathiri mtiririko wa ushahidi wa kesi ya msingi, baada ya kupima maelezo yote hayo sijapata shaka ya msingi kwamba kulikuwa na nguvu katika kutoa maelezo hivyo nimeamua niipokee hii statement (kielelezo) kiwe sehemu ya ushahidi na pingamizi hili linatupiliwa mbali,” alisema Jaji Matupa.
Maamuzi hayo ya Jaji Matupa yalitoa fursa kwa kesi ya msingi kuendelea kusikilizwa kwa shahidi wa 16 wa upande wa jamhuri kuendelea na ushahidi wake ambapo aliruhusiwa kuyasoma maelezo ya onyo ya mshitakiwa wa sita Abdalla Petro yenye kurasa 24 yakielezea namna ambavyo mshitakiwa huyo alivyoshiriki katika tukio la mauaji ya marehemu Barlow na mengine ya uhalifu wa kutumia silaha jijini Mwanza.
Shahidi huyo alifunga ushahidi wake na Jaji Matupa kuhairisha kesi hiyo ambapo itaendelea kesho kwa ajili ya kusikilizwa na shahidi wa 17 upande wa mashitaka atatoa ushahidi wake mahakamani hapo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.