Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais wa Marekani amejiuzulu kutokana na madai kuwa alikuwa na mawasiliano na serikali ya Russia.
Ikulu ya Marekani White House imethibitisha kujiuzulu kwa Michael Flynn na kutangaza kuwa jenerali wa jeshi mstaafu Keith Kellog anakaimu kwa muda nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Flynn.
Katika barua yake ya kujiuzulu, Michael Flynn amesema alitoa taarifa pungufu kwa Makamu wa Rais Mike Pence, ambaye katika mahojiano mubahsara aliyofanyiwa na televisheni ya nchi hiyo alikanusha madai yaliyotolewa dhidi ya jenerali huyo mstaafu wa jeshi.
"Nilimtaarifu bila kukusudia Makamu wa Rais mteule na wengineo taarifa zisizo kamili kuhusu mazungumzo yangu ya simu na balozi wa Russia. Nimeomba radhi kwa Rais na Makamu wa Rais kwa udhati wa moyoni, na wamekubali ombi langu la msamaha", imeeleza sehemu ya barua hiyo ya Flynn.
Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence. |
Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais wa Marekani amejiuzulu saa kadhaa tu baada ya kusambaa ripoti kuwa mwezi uliopita Wizara ya Sheria ilitoa indhari kwa Rais wa nchi hiyo Donald Trump kwamba Flynn alisema uongo kuhusu mawasiliano aliyofanya na balozi wa Russia mjini Washington na kwamba kulikuwa na hatari ya yeye kutumiwa na serikali ya Russia kufanya usaliti.
Mazungumzo hayo ambayo yalifanyika kabla ya Trump kutawazwa kuwa rais wa Marekani yalilenga kuhusu kuondolewa vikwazo Russia ambavyo iliwekewa na serikali ya rais wa wakati huo wa Marekani Barack Obama.
Flynn ni mmoja wa maafisa waandamizi wa serikali mpya ya Marekani ambaye ni maarufu kwa chuki dhidi ya Uislamu.../
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.