ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, February 3, 2017

KOREA KASKAZINI YAONYA DHIDI YA CHOKOCHOKO ZA SERIKALI MPYA YA TRUMP


SERIKALI ya Korea Kaskazini imetoa onyo kali juu ya chokochoko za Marekani katika serikali mpya ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Pyongyang mapema leo sanjari na kuonya juu ya hatua za Washington kufanya maneva ya kijeshi kwa kuishirikisha Korea Kusini na ambayo hufanywa kila mwaka  imesema kuwa, Washington na Seoul zinaifanya hali ya mambo katika Peninsula ya Korea kuwa mbaya sana.

Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini
Aidha ripoti hiyo imesema kuwa, maneva hayo ya kijeshi ambayo yamepangwa kufanyika mwezi Machi mwaka huu, mbali na kuvuruga usalama, yanakusudia kurejesha upya silaha za nyuklia za Marekani katika eneo hilo. Radiamali ya Korea Kaskazini juu ya luteka ya pamoja baina ya Korea Kusini na Marekani imetolewa katika hali ambayo tayari Waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis amewasili mjini Seoul kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Korea Kusini kuhusiana na masuala ya kijeshi.

Moja ya silaha hatari za Korea Kaskazini zinazoitia tumbojoto Marekani

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Seoul imesema kuwa, katika safari hiyo ya siku mbili, Mattis atajadiliana na viongozi wa nchi hiyo miradi ya nyuklia na makombora ya balestiki ya Korea Kaskazini na kadhalika suala la uwekaji ngao ya makombora ya Marekani ya THAD nchini humo. Ni vyema kuashiria kuwa, Korea Kusini na Kaskazini zimekuwa katika maandalizi ya kijeshi tangu kumalizika vita baina yao hapo mwaka 1953 huku nchi hizo zikishindwa kutia saini mkataba wa amani baina yao.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.