ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 29, 2016

MAFUNZO YA MPIRA WA KIKAPU KWA WATOTO NA VIJANA YAANZA KATIKA UWANJA WA MPIRA WA KIKAPU KILOLELI MWANZA

Chama cha mpira wa kikapu mkoa wa Mwanza (MRBA) kupitia Kamisheni yake ya Watoto, Vijana na maendeleo ya shule kwa kushirikiana na shirika la kijamii linalojishughulisha na michezo, Planet Social Development (PSD) na timu ya Mwanza Eagles tunaendesha mafunzo ya mpira wa kikapu kwa watoto na vijana katika uwanja wa mpira wa kikapu Kiloleli ambayo yatakuwa yakifanyika kwa siku za jumamosi saa 2 asubuhi, Jumanne na Alhamis kuanzia saa kumi jioni.

Kwa kushirikiana na Kocha Amin Musira ambaye ni kocha wa muda mrefu hapa Mwanza, tumeanza kufundisha watoto hawa wanaotoka/wanaishi maeneo ya karibu na uwanja huu na pia wanaosoma katika shule za msingi za Pasiansi, Kilimani, Kiloleli, Hekima na Muungano na pia shule za Sekondari Kiloleli, Nyamanoro, Pasiansi, Kilimani na zingine zilizo karibu na uwanja huu.

Tumeanza na utaratibu huu kwa sababu watoto hawa wataweza kufika uwanjani bila kutumia usafiri wa gari kwa maana ya nauli kitu ambacho kimekuwa kikwazo kikubwa kwa watoto kufika katika viwanja vya mbali na wanapoishi. Na bahati nzuri ni kwamba uwanja huu upo katikati ya makazi ya watu na ndio sahihi kwani watoto wataweza fika uwanja masaa yote wapatapo nafasi mara baada ya muda wa masomo na shughuli za nyumbani.

Mafunzo haya yanalenga kuibua vipaji vya watoto hawa na kuwaendeleza katika mchezo huu ili tuweze kurudisha mchezo huu katika hadhi yake kama ilivyokuwa awali katika mkoa wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla.

Pamoja na kutambua, kuibua na kuendeleza vipaji vya watoto katika mchezo huu, pia washiriki watapata nafasi ya uelewa kuhusu masomo na michezo na pia michezo na afya ili waweze kusoma kwa bidii na kuwa na afya njema wakati wote. Pia tuna mpango wa kufundisha makocha (walimu) kutoka katika shule za msingi na sekondari za hapa Mwanza ili watoto hawa waweze kupata nafasi ya kujifunza katika vipindi vya michezo wawapo shuleni.

Katika kufanikisha mafunzo haya vizuri, bado tunahitaji kupata vifaa mbalmbali ikiwepo mipira angalau 50 kwa kuanzia, cone, sare/jezi na dawa za huduma ya kwanza.

Hivyo, tunawakaribisha na kuwaomba wadau wajitokeze katika kusaidia kufanikisha mafunzo haya kwa kutoa mahitaji mbalimbali yanayoitajika. Kwa yeyote mwenye kuweza kutupatia vifaa vinavyoitajika afike katika ofisi ya Utamaduni na Michezo ya Manispaa ya Ilemela aonane na Afisa michezo ambae ndie mratibu wa mafunzo haya au afike shule ya msingi Nyanza aonane na Kaimu mwenyekiti wa MRBA Ndg. Juvenile Kaiza ambaye ni mwalimu mkuu wa shule hii ama afike uwanjani Kiloleli.

Imetolewa na:

Kizito Sosho Bahati
Mratibu wa Mafunzo

0764 993 000/0784 970 235

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.