Dk. Emmanuel Nchimbi akitoa malalamiko yake mbele ya vyombo vya habari mara baada ya kutoka kwenye kikao cha CC. |
HABARI CHANZO: MWANAHALISI
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC-NEC) imetoa orodha ya wagombea watano bila ya jina la Edward Lowassa kuwemo ndani. Lakini katika hali inayoonesha mpasuko, baadhi ya wajumbe wa kamati kuu wamepinga uamuzi huo. Anaandika Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Majina yaliyopatikana, ambayo hata hivyo hayajatangazwa rasmi na chama, ni ya Bernard Membe, Dk. John Magufuli, Dk. Asha Rose-Migiro, January Makamba na Balozi Amina Salum Ali.Membe ni mbunge wa Mtama na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Magufuli ni mbunge wa Chato na Waziri wa Ujenzi, Dk. Migiro ni mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Makamba ni mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, na Balozi Amina ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Tume ya Umoja wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa, Marekani.
Maamuzi hayo hayakuwaridhisha baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu hasahasa wanaojulikana kuwa ni waungaji mkono wa Lowassa, na wametokeza hadharani kuyapinga huku wakilalamika kuwa kanuni zimevunjwa.
Dk. Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa wamefika mbele ya vyombo vya habari mara tu kamati kuu ilipomaliza kikao chake usiku huu, na kusema hawakubaliani na kilichotendwa.
Wajumbe hao wakizungumza kwa kupokezana huku wakitoa kauli kali, wamesema kanuni za utendaji katika vikao vilivyotangulia Kamati Kuu zimekiukwa. Kamati Kuu ina wajumbe 32.
Wamesema ukiukaji umekuja pale Kamati Kuu ilipopatiwa majina matano, badala ya kupokea majina yote ya wanachama walioomba kuteuliwa, ili yenyewe ndiyo itoke na majina matano baada ya kuyafanyia uchambuzi.
“Kanuni zinasema Kamati Kuu itapokea majina ya waombaji wote na ikishafanya uchambuzi wa kila muombaji, yakiwemo maoni ya kamati ya usalama na maadili, ndiyo huchagua majina matano yanayofikishwa mbele ya Halmashauri Kuu,” alisema Dk. Nchimbi ambaye alitokea kama kiongozi wa hao wajumbe watatu.
Kimbisa ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, amesema hawakubaliani na maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu kwa sababu hawakutarajia Kamati Kuu itakiukwa na kupokea majina ya baadhi tu ya waombaji.
“Haijawahi kutokea tangu nilipoingia katika Kamati Kuu kushuhudia ukiukaji wa kanuni kama ilivyotokea leo (jana) hii. Tumejitahidi kuuliza kwa mwenyekiti imekuaje kanuni inakiukwa lakini tumekosa maelezo ya kuridhisha,” amesema Simba, waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Wakati wajumbe wa Kamati Kuu walipokuwa wanatoka nje ya ukumbi wa kikao, Nape Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi, aliwaambia waandishi wa habari kikao kimemaliza kazi, tayari anayo majina matano ya waombaji walioteuliwa kupelekwa NEC, lakini “nitayatangaza kesho (leo) saa 4 asubuhi.”
Muda huo ni muda ambao kwa mujibu wa ratiba aliyoitoa mapema jana, kikao cha NEC kimepangwa kuanza. NEC yenye wajumbe wapatao 378 huwa inajadili majina hayo na kupiga kura ili kuchagua majina matatu ambayo hupelekwa mbele ya Mkutano Mkuu kwa uamuzi wa kupata mgombea.
Mgombea wa CCM anatarajiwa kutangazwa mara tu mkutano mkuu ambao utaanza mchana, utakapomaliza kupiga kura. Mkutano Mkuu una wajumbe zaidi ya 2,000.
Kabla ya hapo, itakuwa yametolewa matokeo ya kura alizopigiwa Dk. Ali Mohamed Shein aliyepitishwa kugombea tena nafasi ya urais wa Zanzibar.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.