NA PETER FABIAN, MWANZA.
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo ameonya baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa wanaohamasisha vurugu na uchochezi unaopelekea uvunjifu wa amani.
Akizungumza kwenye mkesha wa kuliombea taifa uliofanyika katika uwanja wa michezo wa CCM Kirumba jana jijini hapa, RC Mulongo alisema kuwa wananchi hawana budi kuendelea kuliombea taifa bila kujali itikadi za madhehebu ya dini zao na itikadi za kisiasa chini ya mfumo wa vyama vingi.
“Wananchi msikubaliane na baadhi ya watu wachache wakiwemo viongozi wa kisiasa wanaotuhamasisha katika misingi ya vurugu, uchochezi na hata tuanze kubaguana kwa madhehebu ya dini zetu, rangi na makabila jambo ambalo tukiruhusu litatuingiza katika taifa lenye vurugu na machafuko na kusababisha amani iliyopo itoweke,”alisema.
Mulongo alisema kuwa kutokana na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Mwana kukumbwa na changamoto mbalimbali za ulinzi na kupelekea imani za kishirikina kuchukua nafasi na kusababisha mauaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi (Albinisimu) kujitokeza.
“Serikali ya Mkoa itachukua hatua ya kukomesha imani hizo potofu na kuwakamata wanaofanya vitendo hivyo vya mauaji kwa kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria pia wananchi mwendelee kuliombea taifa ikiwemo watu wa aina hiyo ili kusaidia taifa kuendelea kuwa na amani na utulivu,”alisisitiza.
RC Mulongo alitumia mkesha huo kuwakumbusha wananchi tukio la kutoloshwa kwa mtoto ambaye anaulemavu wa ngozi (Albino) lililotokea hivi karibuni wilayani Kwimba ambapo uchunguzi wa awali umebaini ndugu wa karibu kuhusika na tukio hilo.
“Tuendelee kumuombea pia mtoto huyo ili apatikane akiwa hai wakati ambapo serikali na Jeshi la Polisi likiendelea kuwatafuta watu waliomwiba kutokana na shindikizo za imani za kishirikina kutawala baadhi ya miyo za watu, lakini wananchi watupatie taarifa za siri zitakazowezesha kumpata mtoto huyo na watu wanaeendesha vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wetu,”alisisitiza.
Awali Askofu Charles Sekelwa kwa niaba ya maaskofu na wachungaji wa madhehebu ya makanisa mbalimbali yaliyopo jijini Mwanza yaliyoandaa mkesha huo wa kuliombea taifa na Mkoa wa Mwanza , alisema wataendelea kumlilia “Mungu” ili kudumisha amani ya taifa iliyopo.
Askofu Sekelwa alisema kuwa hali ya taifa ilivyo inajulikana kutokana na baadhi ya maeneo kukumbwa na vurugu na kusababisha kuashiria kwa machafuko na uvunjifu wa amani kutokana na kukumbwa na changamoto hizo ni vyema kuendelea kuliombea taifa kwa nguvu zote.
“Tushirikiane kuliombea taifa hasa mwaka huu ambapo taifa litakuwa katika upigaji kura za maoni juu ya kupata Katiba mpya na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ili kuendelea kuwa na utulivu na amani, jambo ambalo linatakiwa kupewa kipaumbele na kila mwananchi,”alisema.
Wito ni watanzania wote kuendelea kuliombea taifa na viongozi wa serikali ni kuhakikisha changamoto mbalimbali zilizopo katika kuwapatia huduma na maendeleo wananchi zinafanyiwa kazi haraka ikiwemo kuzisikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi badala ya kuzisikiliza kisha kutozitekeleza kwa wakati jambo linalowatia hofo na mashaka wananchi.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.