NA PETER FABIAN, MWANZA.
HALMASHAURI ya Jiji la Mwanza imesitisha mkataba na Wakala wa ukusanyaji ushuru wa Mabango Kampuni ya Senson Ltd katika maeneo yote ilikokuwa ikikusanya fedha jijini hapa.
Akizungumza na MTANZANIA juzi Ofisini kwake, Mkurugenzi wa Jiji hilo, Halifa Hida, alieleza kuwa uamuzi huo wa kusitishwa kwa Wakala huyo wa Kampuni ya Senson Ltd aliyekuwa ameshinda zabuni ya ukusanyaji ushuru wa mabango katika maeneo yote ya Halmashauri unaanza kutekelezwa Januari Mosi mwaka huu wa 2015.
Mkurugenzi Hida alifafanua kuwa Wakala huyo wa ukusanyaji ushuru alitakiwa kukusanya ushuru wa Sh milioni 56,400,000/= kila mwezi ikiwa ni mkataba alioingia na Jiji hilo baada ya kushinda zabuni iliyokuwa imetangazwa, lakini ameshindwa kufikia malengo ya kiasi alichotakiwa kukusanya na imekuwa ikikusanya fedha kiasi cha chini ya Sh miilioni 30 kwa kila mwezi kinyume na mkataba.
Hida alifafanua kuwa kutokana Kampuni hiyo kuonekana kukusanya chini ya kiwango na kushindwa kuwasilisha fedha alichokubali kwenye mkataba wakati aliposhinda zabuni, Halmashauli inamdai kiasi cha Sh milioni 102,000,000/= ambazo ni ushuru wa mwezi Julai hadi Agosti mwaka 2014.
“Tumesitisha mkataba wa Wakala huyu, lakini tumemwandikia barua ya kumtaka alipe fedha kiasi cha Sh milioni 102,000,000/= zikiwa ni makusanyo ya ushuru na malimbikizo kwa miezi miwili ambayo alikusanya na kuwasilisha kiasi kidogo kinyume na mkataba ,”alisema.
Mkurugenzi alifafanua kuwa tayari hatua ya utekelezaji huo umetakiwa kuanza tangu jana Januari mosi mwaka huu wa 2015 na taarifa zimetolewa katika kikao cha Kamati ya fedha chini ya Mwenyekiti wake Meya wa Jiji, Stanslaus Mabula (CCM) ambaye ni Diwani wa Kata ya Mkolani na Bodi ya zabuni ya Halmashauri hiyo.
“Tunazo taratibu, kanuni na sheria za Halmashauri ya Jiji katika kuingia mikataba na utekelezwaji wake iwapo Wakala wa Kampuni husika iliyoingia mkataba ameshindwa kufikia malengo atakuwa amevunja mkataba na hapo tunageukia sheria inasema nini basi tunaitekeleza kwa kumtaka alipe akishindwa tunamfikisha Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria,”alisisitiza.
Hida amewatahadhalisha wananchi wa Jiji kutolipia ushuru wa mabango kwa Wakala huyo Kampuni ya Senson Ltd, kwani tayari amesitishiwa uhalali wa ukusanyaji ushuru na kuwataka wananchi kulipia ushuru huo katika Ofisi za Halmashauri ya Jiji ili kuepuka kupoteza fedha zao ili kuepuka kulipia tena.
Mkurugenzi Hida, ametoa wito kwa wananchi kulipa ushuru wa mabango na kodi mbalimbali kwa Mawakala walio na sifa na ambao bado wana mikataba ya ukusanyaji na Halmashauri kwa wakati ili kuepuka kulipa na kupigwa faini kutokana na kushindwa kufanya hiyo kwa wakati ili kutekeleza kauli mbiu ya “lipa ushuru kwa maendeleo ya Jiji”.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.