ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, December 30, 2014

HALMASHAURI YA JIJI LA MWANZA KUBOMOA MAJENGO YA SHULE YA MSINGI NYAKABUNGO YALIONEKANA HATARI KWA WANAFUNZI

NA PETER FABIAN, MWANZA.
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Halifa Hida, amemwagiza Idara ya Uhandisi kuyabomoa haraka majengo ya vyumba vitano vya madarasa katika shule ya msingi Nyakabungo jijini hapa.

 Hida akizungumza na MTANZANIA jana Ofisini kwake alisema kwamba baada ya agizo la Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula, alilolitoa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani katikati ya juma lililopita akiwataka wataalamu kwenda kufanya ukaguzi wa kina na uthamini ili kuona kama inafaa kufanya ukarabati aidha kuyabomoa majengo hatarishi.

“Tunatekeleza kwa kuamua kuyabomoa baada ya Injinia Mkuu wa Halmashauri hiyo, Injinia Ezekiel Kunyaranyara na Afisa Elimu kwenda kufanya ukaguzi wamekuja na kushauri kuvunjwa majengo mawili yaliyo na vyumba vitano vya madarasa yaliyo kwenye hatari ya kubomoka na kuwa tishio kwa maisha ya walimu na wanafuzi wa shule hiyo yaliyojengwa wakati wa Mkoloni,”alisema.

Hida alisema kwamba Halmashauri imedhamilia kuboresha miundombinu ya Elimu, Afya na Barabara ili kuwezesha jamii kupata huduma bora kama inavyokusudiwa na serikali kuu, pia kuokoa maisha ya walimu na wanafunzi wanaotumia majengo ya shule hiyo kwa kuyabomoa kabla ya kuleta maafa kutawezesha Halmashauri kuyajenga upya na kuwa katika mazingira mazuri zaidi na si hatarishi kama ilivyo sasa.

 “Tutatumia fedha za makusanyo ya ndani kuanza na ujenzi aghalau vyumba vitatu vya madarasa wakati kukiendelea kujipanga, lakini pia tunakusudia kuwaomba msaada wadau wetu wa maendeleo kutuchangia ili kukamilisha ujenzi huo haraka ili kutoathili wanafunzi kuendelea na masomo na kuhamasisha wazazi nao kushiriki katika ujenzi huu kwa kutoa michango kwa kuzingatia ni shule yao,”alisisitiza.

Mhandisi Kunyaranyara alifafanua kuwa baada ya kutembelea shule hiyo na Afisa Elimu wa Jiji kufanya ukaguzi wa kina kama ilivyo agizwa, tulibaini kuwa eneo lile la shule hiyo asilimia kubwa liko kwenye chemichemi ya maji hali iliyosababisha baadhi ya majengo kupata nyufa kutokana pia na paa za majengo hayo kuezekwa kwa vigae vilivyochoka na kusababisha kuvuja.

Kwa upande wake Meya Mabula, ambaye ni Diwani wa Kata ya Mkuyuni (CCM) alisema kuwa Mkurugenzi Hida ametekeleza majukumu yake kwa vitendo, lakini pia ametumia busara kuhakikisha hayatokei maafa katika shule hiyo ambayo baadhi ya majengo yake ni enzi za Mkoloni.

 “Tamejipanga kuhakikisha tunakamilisha miradi ya maendeleo katika Kata za Igoma, Pamba, Isamilo, Butimba, Mkuyuni, Mkolani, Igogo, Mbugani, Mahina, Buhongwa, Milongo na Nyamagana ikiwa ni Vituo vya Afya, Zahanati, Madarasa, Maabara, Vyoo, Ofisi za Watendaji, Viwanja vya michezo na barabara za Lami, Changarawe na Mawe na kusaidia vikundi vyote.

Mabula alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuwapa ushirikiana Madiwani na Wataalamu wa Halmashauri ya Jiji pia wadau wa maendeleo watuunge mkono huku pia wadau wa usafi na Taasisi na Mashirika na Kampuni za binafsi ziendelee kutuunga mkono tunapozifuata ili kutusaidia, amewata wadau na wananchi kuwapuuza wanasiasa wanaojipambanua kuwamisha juhudi za maendeleo za Jiji hilo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.