ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, November 12, 2014

TAASISI YA DENMARK YAPIGA TAFU NYANGUGE VIFAA AFYA NA TEKNOLOJIA VYA THAMANI YA SH 120 MILIONI

NA PETER FABIAN, MAGU.
TAASISI ya Grenaa Youth Production School (GYPS) ya nchi ya Denmark imempiga tafu Diwani wa Kata ya Nyanguge Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Hilali Elisha kwa kumpatia vifaa vya Afya na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) vyenye thamani ya Sh milioni 120. Vifaa hivyo vilivyotolewa juzi na Elisha ni robota moja ya mashuka ya wagonjwa, robota moja la nguo za madaktari na wauguzi, mashine moja kubwa ya Utrasound, mashine moja ya EKG ya kupimia wagonjwa wa moyo na Komputa 95 na vifaa vyake.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi,wataalamu,walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Nyanguge, shule za msingi za Nyanguge, Nyambiro, Nenge, Chuo cha Tehama na viongozi wa taasisi za dini na vikundi mbalimbali katani humo wakati wa kukabidhi vifaa hivyo.

Elisha alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa changamoto na kero mbalimbali katika Kata hiyo amekuwa akihangaika kutafuta ufumbuzi kwa kushirikiana na wafadhili na wadau mbalimbali ili kusaidia kuzimaliza ikiwa ni pamoja na kuwezesha wananchi kupata huduma bora kwa wakati kama inavyokusudiwa na serikali.

“Kituo chetu cha Afya cha Kata ya Nyanguge kinakabiliwa na changamoto za vifaa tiba hivyo kutolewa kwa mashine ya Utrasound itasaidia wanawake wajawazito kufanyiwa uchunguzi ambao utakuwa wa uhakika na kupewa majibu, lakini wagonjwa wanaosumbuliwa na matatizo ya moyo pia watapimwa na kuwezesha kupata dawa,”alisema.

Elisha alitoa mgawanyo wa Komputa 95 ambapo alisema kuwa Kanisa Katoriki (RC) litapata moja, Kanisa la Free Pentekoste Tanzania (FPCT) moja, Kanisa la Wasabato (SDA) moja, Kikundi cha Nyagunge Tupendane (NYATU) moja, Taasisi ya Mazingira(RAFE) moja, kikundi cha wakulima na wafugaji kuku (NYAKUKI) moja na kikundi cha mikopo moja.

Komputa zingine zimetolewa kwa shule ya Sekondari Nyanguge (40), Chuo cha Maendeleo Nyanguge (15), Ofisi ya Afisa Tarafa ya Kahangara (1), shele za msingi za Nyanguge (10), Nyambiro (10) na Nange (10), Kituo cha Polisi Nyagunge (2) na zingine NGOs zitakaojitokeza.

Aidha Elisha aliwataka wananchi kuendelea kumpatia ushirikiano kwani wafadhili hao wako katika mchakato wa kujenga madarasa matatu katika Chuo cha Maendeleo Nyanguge ili kutoa huduma kwa vijana wanaojitokeza kusoma hapo, lakini pia aliwahakikishia wananchi kuwa utekelezaji wa mradi wa maji utakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jackiline Liana, alimpongeza Diwani Elisha kwa juhudi zake za kuwaletea wananchi wa Kata yake maendeleo pamoja na kujitolea kwake kuzitafutia ufumbuzi kero za wananchi kwa kutafuta wafadhili mbalimbali ili kuhakikisha huduma zinapatikana.

Kauli hiyo ya Liana ilitolewa na mwakirishi wake Afisa Tarafa wa Kahangara, Thomas Makolobela, alisema kwamba kutolewa na kukabidhiwa kwa vifaa hivyo kutachangia upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa afya kwa wananchi na wanafunzi kupata maarifa kwa kutumia teknolojia ya komputa iliwa ni vitendo.

“Diwani huyu anatekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa vitendo na amekuwa msitari wa mbele kuhakikisha kero na matatizo ya kijamii yanatafutiwa ufumbuzi wa haraka lakini pia huduma kwa wananchi zinapatikana katani humo ili kuwapunguzia wananchi umbali wa kuzipata,”alisema.

Naye Mganga wa Nkuu wa Kituo cha Afya cha Nyanguge, Inocent Charles, alisema kwamba poamoja na kituo hicho kupata mashine hizo hakina wataalamu wa kuzitumia hivyo amemuomba Diwani Elisha kupeleka ombi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu la kuajiri mtaalamu wa kutumia mashine hizo ili kuwezesha wananchi kupata huduma kituoni hapo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.