ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, October 1, 2014

WANAFUNZI 40 WA SEKONDARI YA KABUHOLO KATA YA KIRUMBA WAJERUHIWA KWA RADI MWANZA

Mwanafunzi Goefrey Dionizi wa kidato cha nne wa sekondari ya Kabuholo Kata ya Kirumba wilayani Ilemela jijini Mwanza akiwa anapatiwa matibabu na muuguzi katika Hospitali ya Mkoa ya Seko-toure leo baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa na radi shuleni.
Baadhi ya mwanafunzi wakiwa katika moja ya chumba cha kupatiwa matibabu Hospitali ya Mkoa wa Seko-toure, huku mwanafunzi Joyce Juma(19) wa sekondari ya Kabuholo Kata ya Kirumba wilayani Ilemela jijini Mwanza akiwa amelazwa baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa radi leo asubuhi akiwa shuleni.
Mwanafunzi Goefrey Dionizi wa kidato cha nne wa sekondari ya Kabuholo Kata ya Kirumba wilayani Ilemela jijini Mwanza akipelekwa kulazwa wodini kwa matibabu zaidi baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa na radi sehemu ya mguu wa kulia akiwa shuleni 
Mhudumu wa afya akiwafariji wazazi wa wanafunzi wa shule ya sekondari Kabuholo, waliofika Hospitali ya Mkoa ya Seko-toure kwaajili ya kupewa matibabu baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa na radi wakiwa shuleni.

MWANZA
WANAFUNZI wapatao 40 wakiwemo wa  kidato cha tatu na nne nne wa Shule ya Sekondari ya Kabuholo Kata ya Kirumba wilayani Ilemela mkoani Mwanza wamejeruhiwa leo kwa kupigwa na Radi wakiwa madarasani kufatia mvua kubwa iliyoambatana na radi mkoani Mwanza.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa 1:45 asubuhi wakati wakiwa darasani huku mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha na radi kupiga shuleni hapo katika madarasa mawili ya kidato cha nne A na B na kusababisha baadhi ya wanafunzi kujeruhiwa na wengine kuanguka kutokana na mshituko.

Mwanafunzi Yohana Zabron (19) wa kidato cha nne akielezea njinsi tukio hilo lilivyotokea amesema baada ya kuingia darasani saa 1: 45 mvua kubwa ya upepo ilianza kunyesha huku radi ikipiga na kusababisha wanafunzi kupiga makelele kwa hofu.

Kutokuwepo kwa miundo mbinu ya kuzuia radi (Earth rod) kwa majengo ya Shule ya sekondari Kabuholo pamoja na baadhi ya wanafunzi kumiliki simu kwa kificho wanazozitumia kwa mawasiliano na kusikiliza redio imetajwa kuwa ndiyo chanzo kikuu cha radi kuelekea shuleni hapo na kuleta madhara. 
Mwalimu mkuu shule ya Sekondari Kabuholo Lukanyubilu Nhyanya akiwa katika darasa ambalo wanafunzi wake walikumbwa na radi.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo Lukanyabilu Nhyanya ameeleza kuwa baada ya kusikia kelele za wanafunzi na wengine kukimbilia ofisi ya walimu kuomba msaada alikwenda kufatilia na kukuta baadhi ya wanafunzi wakiwa wameanguka chini na kupoteza fahamu na wengine wakilalamika juu ya maumivu ya kichwa na kifua. BOFYA PLAY UMSIKILIZE MWALIMU


Radi imefumua hapa.
WAKATI HUO HUO
Kaimu Mganga mkuu mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa ya Seko-Toure, Dr Brayn alikiri kupokea taarifa ya kuwapokea wanafunzi wa shule ya sekondari Kabuholo na kueleza wanapatiwa matibabu kufatia tukio la kupigwa na radi wakiwa shuleni. 

Naye Muuguzi wa zamu wa Hospitali hiyo, Aquilina Shayo alieleza kuwa wanafunzi waliofikishwa na kupokelewa hospitalini hapo ni 22 na kupatiwa matibabu na wanafunzi 17 wakionekana kupata mshituko wa kama shoti ya nguvu ya umeme ambapo wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa, watano wameonekana kujeruhiwa na kulazwa kwa matababu zaidi.
Baadhi ya watoto kabla ya kujeruhiwa walikuwa wameketi hapa.
Shayo aliwataja wanafunzi waliolazwa ni Joyce Juma (19) amejeruhiwa mgongoni, Geofrey Dionizi (19) amejeruhiwa mguu wa kulia na Neema Deus (16) amejeruhiwa kifuani wote wa kidato cha nne na Hawa Mussa (16) naye kifuani wa kidato cha tatu.

Wengine waliotibiwa kuruhusiwa kuondoka ni Lucy Jonas, John Bwire, Yohana Zabron, Mohamed Edwin, Frank Cuthbert, Aisha Juma, Asimwe Joseph, Anitha Robert, Lucy David, Anastazia Amon, Marha Zakaria, Faraja Richard, Frola Magesa na David Samike huku wanne ambao hawakufahamika majina yao wakiwa wamefikishwa na kuonekana kutoathiliwa zaidi na kuchukuliwa na wazazi wao na wengine wao kupelekwa Hospitali nyingine
Hakuna masomo wanafunzi wameruhusiwa kwenda majumbani.
Hii ni sehemu ya madhara ya mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Mwanza ambapo pamoja na kuharibu baadhi ya miundo mbinu ya barabara pia imeharibu baadhi ya mabango yanayotumika katika kutangaza matangazo ya biashara  kama hili la barabara ya Makongoro.  

Tukio jingine kama hili limetokea katika shule ya msingi Mahina Kata ya Mahina wilayani Nyamagana ambapo halikuleta madhara yoyote pamoja na kuwepo taarifa za radi kupiga shuleni hapo wakati wanafunzi wakiwa madarasani.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.