ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, October 27, 2014

ESTHA BULAYA ATIKISA UPINZANI KATA YA MAHINA APOKEA WANACHAMA WAPYA 215










NA PETER FABIAN, MWANZA.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) na Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) Kata ya Mahina wilayani Nyamagana mkoani Mwanza, kimevuna wanachama wapya zaidi ya 215 kutoka vyama vya upinzani na kufungua mashina mapya mawili katani humo.

Wanachama hao wapya wamepokelewa na Mbunge wa Viti maalumu (CCM) wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Estha Bulaya, baada shughuli ya kuzindua mashina ya Mahina Mashariki na Nyanguruguru kisha kupokea wanachama hao kutoka vyama vya upinzani vya CUF na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Bulaya alisema CCM kimekuwa Chama pekee kikongwe Barani Afrika ambacho kimekuwa ni kimbilio la wengi kutokana na utaratibu na misingi iliyowekwa na waasisi wa Chama hicho chini ya uongozi wa Hayati Mwl Julius Nyerere ambaye alipewa heshima ya kuwa Baba wa Taifa baada ya utumishi wake wa kuwa Rais wa kwanza wa Taifa hili na Mwenyekiti wa CCM.

Kada huyo wa CCM alisema kuwa vijana wa Chama hicho ni vyema wakamuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwl Nyerere kwa kufanya kazi za kujitolea ikiwemo kushiriki kwenye ujenzi wa vyumba ya Maabara katika shule za sekondari za Kata zilizopo maeneo mbalimbali ya Kata hapa nchini ikiwa ni kumuenzi kwa vitendo.

“CCM kwa sasa inaye Katibu Mkuu wake Abdulhaman Kinana  ambaye amekuwa akizunguka nchi nzima katika Kata Wilaya za Mikoa mbalimbali na kushirikiana na wananchi katika shughuli za ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo vyumba vya maabara kama ilivyokuwa wakati wa uhai wa mwaasisi wetu Baba wa Taifa hayati Mwl Nyerere”alisema.

Bulaya amewataka vijana kujitokeza na kujitolea kushiriki katika shughuli za ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo shule za sekondari za Kata ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kuboresha elimu kutokana na changamoto zinazoikabili Sekta hiyo badala ya kuwasikiliza wanasiasa wa upinzani ambao wamekuwa wakizibeza na kuzipatia majina mengi.

“Wanasiasa wa upinzani wemekuwa wakiziita yeboyebo, zimamoto, na bora liende huku wao pia wamekuwa hawawapi nafasi watoto wao kusoma shule hizo na wamekuwa wakiwapeleka  katika shule za “Asante Nani” hivyo ni watu ambao hawatakii mema kwani wamekuwa wakiwazuia wananchi kuchangia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa maabara” alisema.

Bulaya aliwataka vijana ndani ya CCM kujitokeza kuwania uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa udiwani na ubunge mwakani kwani CCM inao vijana wengi waliokatika misingi inayowawezesha kuomba nafasi kisha kuchujwa na kuwapata wagombea watakaopeperusha bendera ya CCM ili kukipatia ushindi.

Mbunge huyo awaliwataka wananchi na wanachama wa Chama hicho kumuunga mkono Katibu Mkuu Kinana katika harakati zake za kushirikiana na wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii anapopita kwenye ziara za kukagua utakelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM na kusikiliza kero na matatizo ya wananchi.

Bulaya alisema taifa bado linazo changamoto nyingi ikiwemo za huduma katika sekta zote za utoaji huduma kwa jamii lakini kupitia serikali ya CCM iliyopo madarakani imeendelea kuzitafutia ufumbuzi ili kuhakikisha zinapungua na kumalizika ili wananchi waendelee kukiamini Chama hiki kikongwe na kukipa lidhaa tena katika chaguzi zijazo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.