GEITA: Hofu ya usalama wa raia na mali zao imetanda baada ya askari polisi wawili kuuawa na bunduki 10 aina ya SMG kuporwa katika kituo kikuu cha Polisi wilayani Bukombe mkoa wa Geita.
Uporaji huo umefanywa na watu ambao hawajafahamika baada ya kuvamia kituo hicho saa 9:45 alfajiri na kuwashambulia askari polisi waliokuwa zamu na kufanikiwa kuwaua wawili na kujeruhiwa wengine watatu.
Mbali na kupora SMG 10, pia inadaiwa wamefanikiwa kupora risasi ambazo idadi yake haijatambulika mara moja pamoja na mabomu ya kutupa kwa mkono na kutokomea kusikojulikana.
Hili ni tukio la pili katika kipindi miezi mitatu ambapo June 11 mwaka huu askari polisi mmoja aliuawa baada ya watu wasiojulikana kuvamia Kituo Kidogo cha Polisi cha Kimanzichana mkoani Pwani kisha kupora bunduki tatu aina ya SMG na risasi zake.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Joseph Konyo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uvamizi huo umetokea saa 9:45 alfajiri baada ya askari waliokuwa doria kushambuliwa kwa bomu kupitia dirisha la chumba cha mapokezi (CRO) kituo hapo na kisha kuwashambulia kwa risasi askari hao.
Amewataja askari waliouawa kuwa ni WP 7106 Uria Mwandiga na G. 2615 PC Dustani Kimati na waliojeruhiwa askari namba E.5831 CPL David Ngupama Mwalugelwa aliyejeruhiwa kichwa na usoni huku akiumizwa mdomo na meno mawili kungooka pamoja na Mohamed Hassan Kilomo amabye amejeruhiwa kifuani na mguu wa kulia kwa risasi.
IGP atua eneo la tukio:
Kutokana na tukio hilo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, amefika wilayani humo akiwa ameambatana na Kamatio ya Ulinzi na usalama ya Mkoa wa Geita ikongozwa na mwenyekiti wake mkuu wa mkoa wa Geita Saidi Magalula.
IGP Mangu ameagiza askari polisi wa mikoa ya jirani ya Tabora, Shinyanga, Kagera, Mwanza na Kigoma kushirikiana na askari wa Geita kuwasaka wausika ili pamoja na kurejesha silaha zote zilizoporwa.
Agizo la IGP kuwataka askari wa mikoa ya jirani kusaidia msako huo ni kutokana na asilimia 60 ya eneo hilo la wilaya ya Bukombe kuwa na misitu mikubwa.
Amesema msako huo utasimamiwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Isaya Mungulu ambaye aliwasili wilayani Bukombe kwa helkopta ya Polisi saa 11: 39 jioni tayari kwa kuanza msako huo.
IGP Mangu atangaza dau la Sh milioni 10 kwa mtu atakayesaidia kukamatwa kwa wavamizi hao ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa silaha zilizoibiwa.
Mganga Mkuu wa Wilaya:
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Bukombe, Dk. Honorata Rutatinisibwa amekiri kupokea maiti za askari wawili na majeruhi wawili.
Alisema hali za majeruhi zilikuwa mbaya hivyo zilihitaji matibabu zaidi na kulazimika kuwahamishia hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.