Musoma
Chama cha soka mkoani Mara, FAM kimepata pigo kubwa kufuatia kifo cha mwenyekiti wake Fabian Samo, kilichotokea jumanne asubuhi katika hospitali ya mkoa wa Mara mjini Musoma.
Samo ambaye alichaguliwa kushika wadhifa huo, kwa mara ya pili mfululizo katika uchaguzi mkuu uliofanyikia Shirati, wilayani Rorya Novemba 13 mwaka jana baada ya kumshinda mpinzani wake Sospeter Masambu, ameelezwa na baadhi ya wadau wa soka wa mikoa ya Mwanza na Mara kwamba alikuwa ni nguzo na mhimili mkubwa katika kuendeleza fani ya mchezo wa soka.
Katibu wa Chama cha Soka mkoa wa Mara Mugisha Galibona, amesema marehemu Fabian Samo atakumbukwa kwa mengi, ikiwemo msimamo wake katika maamuzi na makubaliano na zaidi alikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kiwango cha soka mkoani Mara kinapanda.
Galibona pia amedai marehemu Samo, alikuwa ni kiungo muhimu baina ya viongozi wa juu wa shirikisho la soka nchini TFF, na wadau mbalimbali wa soka hasa pale timu za mkoa huu zilipokuwa zikisafiri nje ya mkoa katika mashindano ya kombe la taifa na mashindano ya vijana chini ya miaka 17, ya Copa Coca Cola.
Kwa upande wake, mjumbe wa kamati ya utendaji ya TFF anayesimamia masuala ya soka katika mikoa ya Mwanza na Mara, Samwel Nyalla akizungumza na Mwandishi wa BROGU hii kwa njia ya simu kutoka Mwanza amesema, amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha kiongozi huyo kwani alikuwa bado akihitajika kwa mawazo na michango yake mbalimbali katika kuendeleza mchezo wa soka.
Aidha, mjumbe wa kamati ya soka la vijana na wanawake mkoa wa Mara Shomari Binda, akielezea mchango wa marehemu Samo katika medani ya soka, amesema kiongozi huyo ataendelea kukumbwa daima kwa jinsi alivyosimamia maendeleo ya soka la vijana na wanawake kwa kutoa miongozo mbalimbali katika kutaka kufanikisha.
Binda amesema kabla ya kufikwa na mauti marehemu fabian Samo licha ya kuwa katika maradhi alikuwa akifatilia maendeleo ya timu ya vijana ya mkoa wa Mara iliyo na umri chini ya miaka 17 iliyokuwa jijini Dar es salaam kwa ajili ya ushiriki wa mashindano ya Copa Coca Cola ambayo ilitolewa katika hatua ya robo fainali na vijana wenzao wa Mkoa wa Morogoro.
Naye mwenyekiti wa chama cha soka wilaya ya Musoma mjini, aliye pia mjumbe wa mkutano mkuu wa TFF David Sungura amesema kifo cha marehemu Fabian Samo kimekuja wakati timu ya Polisi Mara ikiwa bado inahitaji mchango wake wa mawazo katika maandalizi ya michezo ya ligi daraja la kwanza iliyopata nafasi hiyo hivi karibuni..
Marehemu Fabian Samo atazikwa siku ya ijumaa saa saba mchana nyumbani kwake katika kata ya Nyakato Manispaa ya Musoma baada ya shughuli za ibada na wadau wa soka kutoa heshima zao za mwisho.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.