Kwa kuzingatia hayo, mechi muhimu zaidi kesho Jumapili ni ile inayozikutanisha Manchester City na Queen Park Rangers (QPR), mchezo unaofanyika Etihad, nyumbani kwa City mbele ya washabiki wake. Mechi nyingine inayotia wadau matumbo joto ni ile ya Manchester United na Sunderland, United safari hii wakichezea ugenini.
Ili City watwae ubingwa wanatakiwa kuwa na matokeo kama ya United au mazuri zaidi. Kwa kifupi ni kwamba, City wakishinda kuna uwezekano mkubwa wa kutangazwa wafalme wa soka wa England.
Ni katika hali hiyo Kocha Mkuu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson anasema wao wanaombea litokee jambo la 'kijinga' dhidi ya jirani zao (Manchester City) ili wanyakue tonge mdomoni mwao.
Lakini ikumbukwe kwamba vijana hao wa Roberto Mancini katika msimu wote wamepoteza pointi mbili tu katika uwanja wao huo wa Etihad, yaani wameshinda mechi zote isipokuwa mbili tu walizotoka sare. Ndiyo maana washabiki wao wengi wana matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa walioupata mara ya mwisho mwaka 1968.
Wanachotegemea dhidi ya QPR ni ushindi tu. QPR wananolewa na kocha wa zamani wa City, Mark Hughes aliyetupiwa virago Desemba 2009 baada ya kushinda mechi mbili tu kati ya 11 City walizocheza mfululizo. Kocha huyo pia ameichezea United na Ferguson anamtegemea 'amsaidie kuiangamiza City'. Kwa ujumla timu mbili hizi za Manchester zinatarajiwa kuibuka na ushindi kwenye mechi zao hizi za mwisho.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.