ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, December 4, 2011

'TAIFA BORA LA KESHO LINAANDALIWA LEO' ASEMA AFANDE JOSEPH

WAKAZI wa Jiji la Mwanza na viunga vyake, wametakiwa kushirikiana kwa pamoja katika kutokomeza vitendo vya kifalifu, ili kuimarisha amani, utulivu na ustawi wa jamii.Rai hiyo imetolewa na Ofisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, kutoka kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Joseph Mangapi, wakati alipokuwa akizungumza kwenye mahafali ya Shule ya awali ya Unguja Junior Academy iliyopo Mabatini jijini hapa.

Mangapi alisema, wananchi wote hawana budi kupiga vita vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na baadhi ya watu wasiowaaminifu katika maeneo mbali mbali, hivyo ni vema jamii ikawa mstari wa mbele kutoa taarifa kwa jeshi la polisi dhidi ya wahalifu.

Kwa mujibu wa Ofisa mwandamizi huyo wa jeshi la polisi, kitengo cha Upelelezi Makosa ya Jinai, madhara ya kutokuwa na usalama mahali pa kuishi yanasababisha amani kutoweka pamoja na kuzorota kwa uchumi na maendeleo ya jamii.


"Kwanza naupongeza sana uongozi wa shule hii ya awali ya Unguja Junior Academy kwa mafunzo yenu mazuri kwa watoto wetu. Lakini suala la kudhibiti uhalifu lipo kwa jamii yote.

"Tunapowekeza kwenye elimu, tuwekeze pia katika ulinzi wa nchi na maeneo yetu tunayoishi. Tushirikianeni kufichua wahalifu, na toeni taarifa za wahalifu kwa jeshi lenu la polisi ili watu hao wachukuliwe hatua za kisheria", alisema Mangapi.

Hata hivyo, aliupongeza uongozi wa shule hiyo ya awali ya Unguja Junior Academy iliyopo Mabatini jijini Mwanza, kwa kazi yake nzuri ya kuwalea kwa maadili mazuri watoto wanaosoma shuleni hapo.

Akisisitiza zaidi katika hilo, Mangapi alisema: "Elimu ndiyo mhimili mkubwa wa taifa, pia ndiyo msingi bora wa kila Mtanzania. Hongera sana viongozi wa shule hii ya Unguja Junior Academy kwa kuamua kuwekeza katika sekta hii nzuri ya elimu".


Awali, akisoma risala ya shule, Mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, Michael Joseph Jairo Aridi alisema licha ya elimu bora kutolewa shuleni hapo, lakini kituo hicho kinakabiliwa na upungufu wa viti, meza pamoja na madawati ya wanafunzi.

Alisema, mbali na hayo, shule hiyo ya Unguja Junior Academy inakabiliwa pia na tatizo la uhaba wa fedha za kujiendesha ikiwa ni pamoja na ufinyu wa eneo, na alitoa wito kwa Serikali na wadau kushirikiana na uongozi wa shule hiyo katika suala zima la kuiboresha kwa faida ya maendeleoya taifa.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.