ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, September 23, 2011

BP YANYWEA KWA SERIKALI, KUPEWA LESENI KWA MASHARTI

KAMPUNI ya uuzaji wa mafuta ya BP imesalimu amri kwa Serikali, hivyo kuamua kuondoa mahakamani shauri la kupinga kufungiwa kwake na badala yake kurejea katika meza ya mazungumzo, hivyo kupewa masharti manne inayopaswa kuyatekeleza kabla ya kurejeshewa leseni kuendelea na biashara hiyo.

Masharti hayo yanatokana na kampuni hiyo kukaidi agizo la Serikali la kushusha bei ya mafuta iliyotolewa Agosti mwaka huu, na badala yake kufunga vituo vyake vyote, hali iliyochangia uhaba mkubwa wa mafuta nchini. Hatua hiyo ilisababisha Serikali kutoa amri ya kufunguliwa kwa vituo hivyo katika muda wa saa 24, amri ambayo BP iliendelea kuikaidi, hivyo kupokwa leseni yake.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, BP ilikuwa miongoni mwa kampuni zilizokuwa zikisambaza mafuta nchini, lakini baada ya kushushwa kwa bei ya bidhaa hiyo kampuni hiyo iligoma, badala yake ikakimbilia mahakamani.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Masebu alisema kutokana na hasara waliyopata, BP wamelazimika kufuta kesi na kutaka kuingia kwenye kikao cha majadiliano kilichohitimisha malumbano yaliyokuwapo kwa kuwapa masharti manne kabla ya kuwarudishia leseni.

Chanzo cha mvutano
Mvutano baina ya Serikali na BP ulianza Agosti 3, mwaka huu baada ya Ewura kupitia kwa Masebu ilipotangaza kushusha bei ya mafuta mjini Dodoma ambapo petroli ilishuka kwa Sh202.37 kwa sawa na asilimia 9.17.

Katika tangazo hilo, dizeli ilishuka kwa Sh173.49 sawa na asilimia 8.32 na mafuta ya taa yalishuka bei kwa Sh181.37, sawa na asilimia 8.70. Masebu alisema kushuka kwa bei hizo kulitokana na kukamilika kwa mchakato wa kuandaa kanuni mpya ya ukokotoaji wa bei za bidhaa za mafuta hasa kutokana na maagizo ya Serikali na pia, kubadilika kwa viwango vya kodi katika bidhaa za mafuta.

Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa, kodi za mafuta ya taa ziliongezwa na pia kupunguzwa kwa kodi za mafuta ya dizeli na tozo za mamlaka mbalimbali zimetazamwa na kupunguzwa.


CHANZO www.mwananchi.co.tz

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.