Polisi wamesema kuwa guruneti hilo lilirushiwa watu waliokusanyika katika kituo cha basi muda mfupi baada ya tume ya uchaguzi nchini humo kumtangaza Paul Kagame kama Rais kwa ushindi wa zaidi ya asilimia 93 ya kura.
Bado haijajulikana ni nani aliyehusika na shambulio hilo japo watu watatu wametiwa nguvuni na wanasaidia polisi na uchunguzi.
Hili ni shambulio la nne la magruneti katika miezi minne mjini Kigali na yanashukiwa kuhusika na uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
HABARI KUHUSU UCHAGUZI:
Katibu mtendaji wa tume ya taifa ya uchaguzi huo Charles Munyaneza alisema mgombea wa RPF Paul Kagame alichaguliwa kwa asilimia 93 ya kura zote zilizopigwa.
Mpinzani wake wa karibu Dr Jean Dascene Ntawukuriryayo ameshika nafasi ya pili akiwa na asilimia 5, Prosper Higiro amepata asilimia 1.3 naye Dr Alivera Mukabaramba amepata asilimia 0.4 ya kura.
Tume ya taifa ya uchaguzi imesema mgombea yeyote anayepinga matokeo hayo ana muda wa saa 48 kupeleka malalamiko yake kabla ya tume hiyo kuidhinisha na kuyatangaza rasmi.
Lakini haitarajiwi kuwepo malalamiko yoyote kwani wagombea wengine wamekubali kushindwa na kutoa risala za pongezi kwa mshindi Rais Paul Kagame.
KWA HISANI YA BBC SWAHILI.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.