ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, December 8, 2025

SIMBACHAWENE: HAKUNA TISHIO LA KUZIMWA INTERNET TANZANIA, HALI YA USALAMA NI SHWARI.

 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema kuwa hatua ya kuzima mtandao wa intaneti nchini ni chaguo la mwisho kabisa, na kwa sasa hakuna sababu yoyote inayoashiria uwezekano wa TCRA kuchukua hatua hiyo kuelekea maadhimisho ya Uhuru kesho, Desemba 09, 2025.

Akizungumza leo, Desemba 08, 2025, Simbachawene amesema kuwa taarifa zinazosambaa mtandaoni kuhusu hofu ya kuzimwa kwa internet hazina msingi, kwani hali ya kiusalama nchini imo katika kiwango cha kuridhisha.

“Kuhusu kuzimwa mtandao, kwa sababu nyenzo kubwa inayotumika na hawa wanaharakati wa mitandaoni ni taarifa za taharuki… mpaka sasa hatujaona tishio lolote la kusema mtandao umekuwa tatizo,” amesema.

Ameeleza kuwa mitandao ya intaneti ina mchango mkubwa katika maisha ya kila siku ya Watanzania, kuanzia shughuli za kibenki, usafiri, mawasiliano hadi huduma mbalimbali za kijamii, hivyo serikali haina sababu ya kuuzuia bila msingi wa kiusalama ulio wazi.

“Tufahamu mtandao huu ndio unatumika kutoa huduma nyingi za kijamii. Kwa hiyo kuzima internet ni chaguo la mwisho sana pale ambapo hali ikiwa mbaya… lakini mpaka sasa, tunaoangalia usalama wa nchi, tunaona hali ni shwari,” amesema.

Simbachawene amesisitiza kuwa hadi sasa hakuna tishio lolote linaloweza kuilazimu TCRA kuzima huduma za intaneti, na Watanzania wanapaswa kuendelea na shughuli zao kama kawaida bila wasiwasi.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment