ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, December 21, 2025

MGANGA MKUU MANISPAA YA KIBAHA ACHARUKA AKEMEA TABIA YA WATUMISHI WANAOFANYA KAZI KWA MAZOEA

 


NA VICTOR MASANGU,KIBAHA

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Dr. Catherine  amekemea tabia ya baadhi ya watumishi kushindwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kuagiza kuimarishwa kwa huduma za wateja katika vituo vya afya ili kuboresha huduma ya matibabu.


Pia ametoa wito kwa kamati za afya kuhakikisha wanaweka misingi mizuri ya  kujadili kwa kina taarifa za takwimu zilizowasilishwa katika kikao cha tathmini ya mwaka 2024/2025 kwa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe.

Hayo ameyabainisha wakati wa kikao hicho cha tatmini kwa kipindi cha mwaka wa 2024/2025 Dkt. ambapo amebainisha kuwa  idara ya afya wanapaswa   kufanikisha ukusanyaji wa mapato kwa kiwango cha asilimia 50 hadi kufikia kipindi cha tathmini.

Kadhalika  amesisitiza kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mikakati madhubuti ya upatikanaji wa bima ya afya kwa wananchi wote, wakianza na kaya zenye mahitaji maalum.

Amesema  kuwa mpango wa bima ya afya kwa wote utaanza kwa kaya ambazo zitachangia kiasi cha shilingi 150,000 kwa mwaka kwa ajili ya baba, mama na watoto, na kuagiza utolewaji wa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kujiunga na mpango huo.

Aidha,  ameongeza kuwa kuanzia Januari 2026, kituo cha afya cha Kilimahewa kianze kutoa huduma rasmi. Alionya kuwa mtu yeyote aliyepokea fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi lakini hawezi kuumaliza, anatakiwa kutoa taarifa mapema kwa uongozi.

 
Kwa upande wake, Mratibu wa Kitengo cha Dharura, Dkt. Majaliwa, alieleza kuwa kuna upungufu mkubwa wa wauguzi katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani, na kueleza kuwa walipo ni wachache na hawapati posho zao kwa wakati. 

Pia amebainisha kuwa madereva wa sekta ya afya pia hukumbwa na changamoto hiyo hiyo ya kucheleweshwa kwa malipo yao.

Naye mwakilishi kutoka Ofisi ya Utumishi wa Umma Happyness Anania akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha  amewataka watumishi kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinafikishwa kwa viongozi wao moja kwa moja.

Ameingeza kuwa lengo kubwa ni kuhakikisha watumishi wanasililizwa  kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi wa kina na kusisitiza suala la  umuhimu wa kubuni njia mpya za kuongeza mapato kupitia sekta ya afya.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment