ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, August 25, 2025

MWANAMKE ASHIKILIWA KWA TUHUMA KUUA MPENZI WAKE KWA WEMBE.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi

MWANAMKE aitwaye Pendo Medusela (37), mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake, Timithoy Magesa (35), kwa kumkata kwa wembe sehemu mbalimbali za mwili wake kutokana na wivu wa kimapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amebainisha hayo leo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 23, mwaka huu, saa tatu usiku katika nyumba ya wageni ya Bwashee, iliyopo Ndala Manispaa ya Shinyanga.

Amesema kabla ya mauaji hayo, Pendo alipigiwa simu na mwanamke mwingine kwa kutumia simu ya marehemu, akimuonya aachane naye kwa madai kwamba ndiye anayempenda. na baada ya muda Timothy alimtafuta Pendo na kumtaka wakutane katika nyumba ya wageni hiyo, ili wazungumze.

“Hata hivyo, walipokutana walianza kugombana kuhusu mwanamke aliyempigia simu, hali iliyosababisha Pendo kutumia wembe aliokuwa nao na kumkata Timothy sehemu mbalimbali za mwili na kuvuja damu nyingi,” amesema Kamanda Magomi.

Ameongeza kuwa, Timothy amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga.

Kamanda Magomi amesema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi na kueleza kuwa mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani, mara baada ya upelelezi kukamilika.

Aidha, amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi na badala yake kutumia njia za amani kutafuta suluhu pindi wanapokumbwa na migogoro ya kimahusiano.


Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment