Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imempitisha Mhandisi Francis Fikiri Mihayo, Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kaskazini, kujumuishwa kwenye orodha ya wagombea wa nafasi ya ubunge wa Jimbo la Kahama Mjini, mkoani Shinyanga, katika mchakato wa ndani ya chama.

Mhandisi Mihayo ni miongoni mwa wagombea saba waliopitishwa kushiriki kura za maoni ndani ya CCM kwa jimbo hilo muhimu.

Wagombea wengine wanaowania kuteuliwa na CCM kuwania ubunge Jimbo la Kahama Mjini ni pamoja na:Sweetbert Charles Nkuba, Jumanne Kibela Kishimba, James Daudi Lembeli, David Anyandwile Kilala, Juliana Kajala Pallangyo na Benjamini Lukubha Ngayiwa.
Kupitishwa kwa Mhandisi Mihayo kunamuweka katika nafasi ya kushindania ridhaa ya wanachama wa CCM kupitia kura za maoni, hatua muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Chama cha Mapinduzi kupitia kwa Katibu wa NEC – Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, kimebainisha kuwa uteuzi wa majina hayo umetokana na uchambuzi makini, kwa kuzingatia uadilifu, uwezo wa uongozi na kukubalika kwa wagombea miongoni mwa wananchi.