NAHODHA wa zamani wa timu ya soka ya taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’, kipa Peter Rufai amefariki dunia leo, Alhamisi ya Julai 3, 2025 akiwa ana umri wa miaka 61.
Hakuna taarifa zaidi juu ya chanzo cha kifo chake, ingawa Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) limepost taarifa ya kuthibitisha msiba huo na kumuenzi; “Ataishi milele mioyoni mwetu, urithi unaendelea kati ya vijiti na zaidi,”.
Taarifa ya kifo chake Rufai inakuja baada ya kifo cha mshambuliaji wa Liverpool Diogo Jota, aliyefariki mapema leo kwa ajali ya gari akiwa na umri wa miaka 28.
Alizaliwa Agosti 24, mwaka 1963 Jijini Lagos na aliibukia katika klabu ya Maduka Stationary mwaka 1980 ambako alicheza hadi 1985 alipohamia Femo Scorpions zote za Nigeria.
Mwaka 1986 alikwenda kujiunga na AS Dragons ya Benin iliyomfungulia milango ya kucheza Ulaya baada ya kununuliwa na KSC Lokeren ya Ubelgiji mwaka 1987 ambako alicheza hadi mwaka 1992 akahamia KSK Beveren.

Mwaka 1993 aliondoka Ubelgiji kwenda kujiunga na Go Ahead Eagles ya Uholanzi ambako alicheza msimu mmoja na kuhamia SC Farance ya Ureno hadi 1997 alipokwenda Hispania alikochezea klabu za Hércules Alicante hadi 1999 na Deportivo La Coruña hadi mwaka 2000 akarejea Ureno kudakia Gil Vicente FC.

Ameidakia timu ya taifa ya Nigeria kuanzia mwaka 1981 hadi 1998 baada ya Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Ufaransa akidaka jumla ya mechi 66 na kufunga bao moja.
Mungu ampumzishe kwa amani. Amiin.
Tupe maoni yako


0 comments:
Post a Comment