
MAKOSA ya kizembe ya safu ya ulinzi jana yaliigharimu Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa kuruhusu mabao mawili ya zawadi kwa wapinzani, Borussia Dortmund ya Ujerumani waliobuka na ushindi wa 4-2 katika mchezo wa Kundi F Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA Uwanja wa TQL Stadium, Cincinnati, Hamilton, Ohio, Marekani.
Kwanza alikuwa ni kipa Ronwen Williams aliyetoa pasi fyongo ambayo ilinaswa na kiungo Felix Kalu Nmecha akaifungia bao la kusawazisha Borussia Dortmund dakika ya 16 kufuatia mshambuliaji Mbrazil, Lucas Ribeiro kuanza kuifungia Mamelodi Sundowns dakika ya 11 – kabla ya beki wa kulia, Khuliso Mudau kujifunga dakika ya 59 kuwapatia wapinzani bao la nne baada ya mshambuliaji Mguinea, Serhou Guirassy kufunga la pili dakika ya 34 na kiungo Jobe Bellingham wa England kufunga la tatu dakika ya 45.
Hata hivyo, Mamelodi ilipambana na kufaniikiwa kupata mabao zaidi yakifungwa na washambuliaji Iqraam Rayners dakika ya 62 na Lebogang Mothiba dakika ya 90.
Mechi nyingine ya Kundi F jana Fluminense ya Brazil iliichapa Ulsan HD ya Korea Kusini mabao 4-2 Uwanja wa MetLife, East Rutherford.
Mabao ya Fluminense yalifungwa na Arias dakika ya 27, Nonato dakika ya 66, Freytes dakika ya 83 na Keno dakika ya 90’+2, wakati ya Ulsan HD yalifungwa na Lee Jin-hyun dakika ya 37 na Um Won-sang dakika ya 45+3.
Msimamo wa Kundi F baada ya matokeo hayo ni Fluminense inaongoza kwa pointi zake nne ikiizidi bao moja tu Borussia Dortmund, wakati Mamelodi Sundowns inahamia nafasi ya tatu ikibaki na pointi zake tatu huku Ulsan iliyopoteza mechi zake zote mbili za awali inashika mkia.
Tupe maoni yako

0 comments:
Post a Comment