ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, June 28, 2025

AIGLES DU CONGO BINGWA MPYA DRC, VIGOGO WOTE, AS VITA NA MAZEMBE WATUPWA NJE CAF

 


TIMU ya FC Les Aigles du Congo (Eagles of Congo) ya Kinshasa imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ijulikanayo kama Linafoot kwa mara ya kwanza katika historia yake baada ya kutoa sare ya kufungana bao 1-1 na TP Mazembe Ijumaa ya jana (Juni 27, 2025) Uwanja wa Kamalondo, Lubumbashi.


Beki Heltone Kayembe alianza kuifungia Aigle du Congo ‘Des Samourais’, (The Samurai) dakika ya 35 akimtungua kipa Baggio Siadi Ngusia, kabla ya Patrick Mwaungulu kuisawazishia TP Mazembe dakika ya 47 akimtungua kipa Nathan Dibu kufuatia kazi nzuri ya Patient Mwamba.

Kipa Nathan Dibu akipongezwa na wachezaji wenzake jana baada ya kazi nzuri kwenye mchezo wa jana dhidi ya TP Mazembe

Kwa matokeo hayo, Aigles du Congo inayofundishwa na Kocha wa zamani wa Tabora United, Anicet Kiazayidi inamaliza na pointi 35 kileleni mwa Linafoot ikifuatiwa na FC Saint Eloi Lupopo ya Lubumbashi pia yenye pointi 33 baada ya mechi 16 kwenye ligi ya timu 12 na zote zinafuzu Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.


Timu ya AS Maniema yenye maskani yake Kindu, jimbo la Maniema iliyomaliza nafasi ya tatu kwa pointi zake 32 inakwenda Kombe la Shirikisho Afrika katika msimu ambao umekuja na mageuzi makubwa katika Linafoot, kwani hata kigogo mmoja wa kihistoria, iwe Mazembe, AS Vita Club ya Kinshasa wala DC Motembab Pembe aliyepenya nafasi tatu za juu.


TP Mazembe yenye maskani yake Lubumbashi chini ya Kocha Msenegal, Lamine N’Diaye, waliokuwa mabingwa watetezi, wamemaliza nafasi ya nne kwa pointi zao 30 nyuma ya Motema Pembe ya Kinshasa iliyovuna pointi 31.

Mmiliki wa FC Les Aigles du Congo, Vidiye Tshipanda Tshimanga akiwa ofisini katika utendaji wa shughuli za kisiasa kama Mshauri wa Rais Felix Tshisekedi Tshilombo

FC Les Aigles du Congo ni klabu iliyoanzishwa na Mfanyabiashara na Mwanasiasa, Vidiye Tshipanda Tshimanga mwaka 2023 yenye maskani yake Jjini Kinshasa, ambaye aliinunua klabu ya Jeunesse Sportive de Kinshasa maarufu kama JSK na kuibadili jina.


Jukumu kubwa la Kisiasa la Vidiye Tshipanda Tshimanga (48) katika chama chake tawala cha United Congo Dynamics (DCU) kwa sasa ni Mshauri wa Rais wa DRC, Felix Tshisekedi Tshilombo juu ya masuala maalum ya kimkakati na msimu huu amefanikiwa kuizima TP Mazembe, timu inayomilikiwa na Mwanasiasa na Mfanyabiashara mwingine maarufu DRC, Moise Katumbi Chapwe (60) ambaye ni kiongozi wa Chama cha Together for the Republic.

Nje ya ofisi, huu ndio mwonekano wa ‘Tajiri’ Vidiye Tshipanda Tshimanga anayemiliki klabu ya Aigle du Congo

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment