ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, March 27, 2025

ATCL, TTCL HALI TETE ZAIDI YA MWAKA JANA, TAASISI ZINAIDAI BILIONI 311.98/- IMO MISHAHARA

 


MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichele amesema watumishi wa umma katika taasisi 269 wanadai Sh. bilioni 311.98 ikiwamo mishahara, gharama za usafiri wa mizigo kwa wastaafu na marupurupu ya kisheria, kwa viongozi wa idara.

Amesema katika madeni hayo serikali kuu inadaiwa Sh bilioni 274.8 mamlaka za serikali za mitaa zinadaiwa Sh 24.54 wakati mashikira ya umma yakiwa yanadaiwa sh bilioni 12.64.

CAG ameyasema hayo leo, wakati akimkabidhi Rais Samia Suluhu Hassan, taarifa ya mwaka ya Taasisi ya Kuzuia Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), pamoja na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Aidha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali  amesema mwaka wa fedha 2023/24, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imepata hasara ya Sh91.8 bilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 62 kutoka Sh56.6 bilioni mwaka uliopita.

CAG Kichere amesema hasara hiyo inatokana na gharama kubwa matengenezo ya ndege na hitilafu za injini ambapo ndege za Airbus zilikaa muda mrefu bila kufanya kazi zikisubiri injini.


“Pia kampuni ilitumia Sh99.8 bilioni ikiwa ni ruzuku kutoka serikalini endapo isingekuwa ruzuku hiyo kampuni ingepata hasara halisi ya Sh191.6 bilioni,” amesema.

Amependekeza kampuni ishirikiane na Serikali katika kufanya utafiti wa njia bora zaidi za uendeshaji wa ndege kwa kuzingatia masuala ya kifedha na kiuchumi kuongeza ufanisi wa uendeshaji.

Kwa upande wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), amesema lilipata hasara ya Sh27.7 bilioni mwaka wa fedha wa 2023/2024. Ongezeko hili ni kutoka Sh4.32 bilioni ya hasara kwa mwaka uliopita.

Hasara hii ya mwaka huu inachangiwa na ongezeko la gharama baada ya kuhamishiwa Mkongo wa Taifa na Kituo cha Taifa cha Data.

“Licha ya kukusanya mapato ya fedha kiasi cha Sh24 bilioni kutoka mkongo hazikuhesabiwa kama mapato ya TTCL bali zilitumika kulipia deni la mkongo, hivyo shirika limeendelea kupata hasara,” amesema.

Amependekeza deni la mkongo wa taifa lilipwe na taifa na mapato yanayopatikana yatumike kuendesha shirika kiufanisi.

Aidha, Shirika la Posta Tanzania lilipata hasara ya Sh23.6 bilioni ambapo ilichangiwa na kushuka kwa mapato kwa asilimia 20.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.