ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, January 22, 2025

LISSU AM'BWAGA MBOWE UCHAGUZI CHADEMA.

Tundu Lissu amechukua usukani wa Chadema, baada ya kumng'oa madarakani Freeman Mbowe ambaye amekiongoza chama hicho kama mwenyekiti kwa takribani miaka 21. 


Mbowe amekuwa wa kwanza kukiri kushindwa na kumpongeza Lissu kupitia mtandao wa X. Timu ya kampeni ya Lissu pia imetumia mtandao wa X kutangaza ushindi wake. 

Matokeo rasmi ya uchaguzi huo uliofanyika Jumanne usiku yanaonesha kuwa Lissu amepata 51.5% ya kura zote dhidi ya 48.3% alizozipata Mbowe. 


Mara baada ya wagombea wakuu Mbowe na timu ya kampeni ya Lissu kutuma salamu za matokeo kupitia mtandao wa X, wakala wa Lissu kwenye uchaguzi huo na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Godbless Lema aliwaambia waandishi wa Habari kuwa Chadema ndiyo imeshinda. "Chama kimeonesha demokrasia iliyokomaa… huu ulikuwa uchaguzi huru n awa haki kabisa, na umerushwa mubashara na vyombo vya habari. 

Watu wote wameliona hilo," amesema Lema. 


 Lissu ampongeza Mbowe 
Mwenyekiti mpya wa Chadema Tundu Lissu baada ya kutangazwa mshindi amesema chama hicho kimeweka kiwango cha dhahabu cha demokrasia ya ndani na kuvitaka vyama vingine vya siasa nchini humoi kuiga mfano wao. 

Lissu amesema uchaguzi huo ulikuwa wa wazi, huru na haki bila mizengwe japo amekiri kuwa kulikuwa na misuguano na kasoro za hapa na pale. "Tumefanya jambo ambalo halijawahi kufanywa toka chama chetu kianzishwe… tumeweka kiwango cha dhahabu – tunawaambia vyama vingine kama vinaweza viige," ameeleza Lissu. 

 Lissu pia alitumia hotuba yake hiyo ya kwanza kama mwenyekiti kumshukuru mtangulizi wake Freeman Mbowe akisema alichukua kjiti cha uongozi wa chama hicho wakiwa na wabunge watano na katika uongozi wake amekifanya kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania. 

 Lissu pia amesema Mbowe ndiye aliyefanikisha uchaguzi wa jana na leo kuwa huru na haki na anastahili pongezi. "Historia ya chama chetu itakapoandikwa, watatambua huu mchango wako mkubwa uliotoa." Mwenyekiti huyo mpya amesema Mbowe hajastaafu na ataendelea kuwa mjumbe wa kudumu wa kamati kuu ya chama hicho kama ambavyo katiba ya Chadema inavyoainisha. 


 Mbowe 'amuagiza' Lissu kutibu majeraha 
Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema anayemaliza muda wake baada ya kushindwa katika uchaguzi na Tundu Lissu amesema mchakato wa uchaguzi huo umekiacha chama hicho na majeraha. 

 Mbowe amesema japo uchaguzi umefanyika katika misingi ya uhuru, haki na uwazi kama ambavyo aliahidi awali lakini amesema mchakato wa kampeni umeacha majeraha na amemtaka Lissu na viongozi wengine waliochaguliwa kuleta maridhiano ndani ya chama. "Mimi niliahidi kuwa kama ningeshinda ningeliunda kamati ya ukweli na maridhiano ili watu wazungumze na kutibu majeraha yaliyoletwa na kampeni … sasa kama mnaniheshimu kama baba, basi nawaagiza Lissu na viongozi wenzako wapya mlete maridhiano baada ya majeraha yaliyoletwa na kampeni," amesema. 

 Mbowe pia amewataka viongozi wapya kusimama na katiba ya chama hicho na kujizui kuwa na kiburi. Kuhusu mustakabali wake kisiasa, Mbowe amesema anachukua likizo na ataendelea kujikita katika kufanya biashara zake na kuendelea kukishauri chama.

 "Nimepewa likizo ya lazima, na nitaenda kwenye biashara zangu nitafute pesa ana nitaendelea kutoa ushauri kwa chama…Nashukuru nimepewa likizo hii kidemokrasia na katika mfumo ambao nimeujenga mwenyewe… kuna watu waliniambia nijitoe kwenye uchaguzi nitaadhirika, nikawaambia nitafia demokrasia." 

Jinsi kampeni zilivyokuwa za vuta nikuvute, rarua nikuraruwe. Kumalizika kwa uchaguzi huu kunahitimisha takribani kipindi cha mwezi mmoja cha kampeni kali kati mwenyekiti Mbowe anayeondoka madarakani dhidi ya makamu wake, Lissu. 

Lissu aliendesha kampeni zake akijielekeza kwenye kuleta mabadiliko ya namna Chadema inavyopendesha shughuli zake za kisiasa. 

 Anamtuhumu Mbowe akidai amebadilika mno tangu alipotoka gerezani alikokuwa ameshkiliwa kwa miezi 8 akikabiliwa kesi ya Ugaidi. 

 Pia anamtuhumu Mbowe kwa kupokea fedha kutoka kwa watu walio karibu na serikali, japo hakuwahi kutoa ushahidi wowote. Mbowe alikuwa akisema kuwa bado ana kazi ya kufanya kukiimarisha zaidi chama huku akimwita Lissu muongo anayewachafua watu bila ushahidi 

 Hata hivyo, wawili hao waliuambia mkutano mkuu wa chama wakati wa kuomba kura kuwa watabakia ndani ya chama bila ugomvi, bila kujali matokeo ya uchaguzi.

 Lakini wafuatiliaji wa masuala ya siasa za Tanzania wanasema kuna hatari ya Chadema kudhoofika na kugawanyika kutokana na tuhuma ambazo viongozi hao wawili walitupiana wakati wa kapeni za uchaguzi.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.