ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 19, 2024

RFO PWANI-TUMEFANIKIWA KUOKOA WANANCHI 2397 MAFURIKO YA RUFIJI NA KIBITI

 


NA VICTOR MASANGU,PWANI 


Kamanda wa Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Pwani  Mrakibu mwandamizi Jenifa Shirima amesema kwamba hadi kufikia leo Aprili 19 wamefanikiwa kuokoa wananchi wapatao 2397 kutoka Wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani ambao walikubwa na mafuriko ya mvua na makazi yao kuzingirwa na maji.

Akizungumza katika mahojiano maalumu kuhusiana na mwenendo mzima wa hali halisi ilivyo kwa sasa  Kamanda huyo alibainisha hali ya makambi ambayo yametengwa kwa ajili ya wahanga yapo salama.






Kamanda huyo alisema kwamba kutokana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha katika maeneo mbali mbali ziliweza kusababisha baadhi ya wananchi kukosa  makazi yao na hivyo serikali kuamua kuwatafutia maeneo mengine ambayo ni salama zaidi.

Alisema kwamba wameweza kufanikisha zoezi la uokoaji wa wananchi hao kwa kushirikiana bega kwa bega na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa lengo la kuwatoa wananchi katika maeneo yaliyozingirwa na maji.

"Kwa sasa wananchi wote ambao tumeweza kufanikiwa kuwaokoa wameifadhiwa na serikali katika makambi maalumu ambayo yapo katika Wilaya ya Rufiji na Kibiti na yapo katika hali salama ", alisema Kamanda Shirima.

Kadhalika alibainisha kuwa tangu zoezi hilo lilipoanza mnano tarehe 9 machi mwaka huu la kuwavusha watu katika maeneo mbali mbali ambayo wanayooshi ili kuwapeleka maeneo salama.

Pia aliongeza kuwa zoezi rasmi kwa ajili ya uokoaji wa watu ambao wanaishi katika maeneo mengine ya mbali lilianza kufanyika kuanzia Aprili 7 mwaka huu hadi kufikia leo hii kufikia idadi ya watu waliookolewa kufikia 2397.

Katika hatua nyingine Kamanda huyo alitoa rai kwa wananchi wa Wilaya ya Kibiti pamoja na Rufiji kuhakikisha wanaondoka katika maeneo hatarishi na kukubali kwenda katika maeneo salama ambayo yametengwa na serikali.

Nao baadhi ya wananchi wa   Wilaya ya Kibiti na Rufiji wameishukuru kwa dhati serikali pamoja na wadau mbali mbali wa maendeleo kwa kuwapatia misaada ya kibinadamu kutokana na kupata mafuriko hayo.

Pia hawakusita kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Pwani pamoja na Kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Pwani kwa kujituma kwa kipindi chote katika kuwasaidia na  kuokoa maisha yao.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.