Salaam za rambirambi zinaendelea kumiminika katika eneo la Karemjee ambako waombolezaji wamekusanyika kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho kwa mwanasiasa huyo aliyezipamba siasa za Tanzania kuanzia ndani ya chama cha CCM na hata pale alipokwenda chama kikuu cha upinzani Chadema wakati wa harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Kila anayepanda jukwaani amekuwa akitoa saalam na kumwelezea kiongozi huyo kuwa mtu aliyeziishi enzi zake na kutenda mambo kwa umakini mkubwa.
Lowassa alikuwa mvumilivu
Waziri Mkuu wa zamani, Joseph Warioba amekumbusha namna alivyokuwa ameshibana na kiongozi huyo akisema Lowassa alikuwa mtu mwenye misimamo na aliyependa kuchapa kazi kwa umakini mkubwa.
"Lowassa alikuwa mvumilivu sana na mimi niliendelea kuwa na uhusiano huo popote alipokuwa, alipokuwa katika CCM, alipokuwa katika serikali alipokuwa katika Chadema, aliporudi hata CCM, uhusiano wetu ulikuwa kama kaka na mdogo wake,"alisema Warioba.
Akizungumza wakati akitoa salamu zake za rambirambi, makamu wa rais Dkt Philip Mpango amesema taifa limempoteza kiongozi aliyekuwa hodari na aliyedhubutu katika kila jambo. Mbali na kutoa pole kwa familia ya kiongozi huyo, makamu wa rais pia alisema hiki siyo kipindi kigumu kwa familia pekee bali kwa taifa zima.
"Kwa kweli ni mmoja wa watoto mahiri sana wa mama Tanzania ambaye alijitoa kwa dhati kulitumikia taifa letu kwa moyo wake wote. Mheshimiwa Lowassa alitumia vyema karama ambazo alijaliwa na mwenyezi Mungu kuwatumikia Watanzania," alisema Mpango.
Wakati wa uhai wake, Lowassa alishika nyadhifa mbalimbalimbalindani ya CCM mpaka serikalini. Aliingia katika baraza la mawaziri wakati wa awamu ya pili ya utawala wa Rais Ally Hassan Mwinyi akiendelea hivyo mpaka wakati wa utawala wa hayati Benjamin Mkapa.
Alijiuzulu kama Waziri Mkuu
Aliteuliwa kuwa waziri mkuu wakati wa utawala wa awamu ya nne wa Jakaya Kikwete nafasi ambayo alidumu nayo kwa kipindi kifupi cha miaka miwili tu, akilazimika kujiuzulu baada ya kuandamwa na kashfa ya Richmond.
"Nadhani tatizo ni uwaziri mkuu kwamba ionekane waziri mkuu ndiye amefanya haya…ionekane kwamba waziri mkuu ndiye amefanya haya tumwondolee heshima au tumwajibishe ..mheshimiwa spika nimetafakari sana kwa niaba ya chama change, kwa niaba ya serikali yangu nimeamua kumwandikia barua rais ya kumwomba niachie ngazi," alisema Lowassa wakati huo.
Lowassa atazikwa mwishoni mwa wiki jimboni kwake Monduli mkoani Arusha, mazishi ambayo yataongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye kwa sasa yuko ziarani Vatican.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.