ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, April 2, 2023

MABASI MATATU YAZUIWA KUSAFIRI JIJINI MWANZA


Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limezuia mabasi matatu kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria kutoka jijini Mwanza kwenda mikoani kutokana na kutokidhi ubora.


Mabasi hayo ni kati ya 60 yaliyofanyiwa ukaguzi leo alfajiri Aprili Mosi, 2023 katika Stendi ya Mabasi yaendayo mikoani ya Nyegezi jijini Mwanza ambapo Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO) Mkoa wa Mwanza, Sunday Ibrahim amesema ukaguzi huo utakuwa endelevu.


RTO Ibrahim amesema ukaguzi uliyofanyika katika mabasi hayo umebaini kuwa yamechakaa matairi, mfumo wa umeme kutofanya kazi kwa ufanisi na kukosa vifaa muhimu ikiwemo mikanda ya kujikinga dhidi ya ajali.


"Nimeagiza mabasi hayo yasiruhusiwe kusafirisha abiria hadi pale yatakapokuwa yamekidhi vigezo. Pia tunasisitiza wamiliki kutoingiza barabarani magari mabovu hasa wakati huu wa Sikukuu kwani inaweza kuhatarisha maisha ya abiria," amesema.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa mbali na kukemea vitendo vya abiria kushangilia mabasi yanayoshindana barabarani, amewataka kutoa taarifa wanapoona dereva anaendesha kwa mwendo wa kasi unaohatarisha maisha yao.


"Abiria tumieni namba za Polisi zilizobandikwa kwenye magari mnayosafiria kutoa taarifa. Pia mkiona mwendo usiyofaa kuweni wa kwanza kumkemea dereva anayefanya hivyo kwa sababu anahatarisha maisha yenu," amesema Mutafungwa.


Kuhusu upandishaji holela wa tiketi, Afisa Ukaguzi kutoka Mamlaka ya Usafirishaji Ardhini (Latra) Mkoa wa Mwanza, Vitalino Ngonyani amewataka abiria kutokubali tiketi zilizoandikwa kwa mkono badala yake wapatiwe tiketi mtandao iliyokatwa kwa kutumia mashine ya POS ambayo ina nauli elekezi.


"Njia pekee ya kukomesha upandishaji holela wa tiketi ni sisi abiria kutokubali kupewa tiketi iliyoandikwa kwa mkono. Tiketi mtandao ndiyo inayotoa bei elekezi ya nauli hasa wakati huu wa sikukuu," amesema Ngonyani


"Abiria tukiachana na ulimbukeni wa kushabikia dereva anapoendesha kwa kasi tutapunguza ajali nyingi nchini, ikitokea mmoja wetu akasimama kukemea tushikamane naye ili kunusuru maisha yetu," amesema Yohana Samwel, Mkazi wa Mwanza 


Naye Mkazi wa Kigoma, Seth Mugambila amelitaka jeshi la polisi kuweka askari kila kituo cha ukaguzi wa magari kwa ajili ya kufuatilia iwapo abiria wote wamepatiwa tiketi mtandao ili kuwaepusha dhidi ya utapeli kwenye nauli za usafiri.

"Kuna baadhi ya mabasi ukienda kukata tiketi wanakuambia mashine imeharibika au hakuna mtandao hivyo ukate kwa kutumia karatasi utabadilishiwa ukishapanda kwenye gari kumbe unatengenezewa mazingira ya kutapeliwa. Wengine ukihoji wanakushambulia hivyo polisi wakague mara kwa mara," amesema.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.