ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, March 6, 2023

HAWA HAPA WALIOPENDEKEZWA KUMRITHI MREMA


Dar es Salaam. Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), umepitisha majina ya wagombea watano wanaotarajiwa kupigiwa kura katika mkutano mkuu kumpata mwenyekiti mpya wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika leo Jumatatu.


Jina la Katibu Mkuu wa Chama hicho Richard Lyimo ni miongoni mwa waliopitishwa wengine ni Mhandisi Aivan Jackson, Stanley Ndamgoba, Felikx Elias na Abuu Changawe.

Uchaguzi huo unafanyika, Dar es Salaam ikiwa ni kuziba nafasi iliyoachwa wazi na  Augustino Mrema aliyefariki dunia Agosti 21 mwaka jana akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu ya afya.


Msimamizi wa mkutano huo, Hamad Mkadam amesema ulitawaliwa na vurugu kiasi cha kusimama mara kwa mara.

Pia Mkadam ambaye ni kaimu mwenyekiti, alilazimika kupitisha majina yote matano baada ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo baada ya wajumbe kugoma kuwakata baadhi ya wagombea.

"Wajumbe wamepitisha majina yote ili wanachama wakachague wenyewe mtu wanayempenda kuwaongoza, hii ndiyo demokrasia yenyewe, wagombea wote wanasifa," amesema.

Amesema kwa msingi huo majina ya wagombea wote watano yatawasilishwa kwenye mkutano huo na wanachama wachague kiongozi wanayempenda.

Hata hivyo, uamuzi wa kupitisha majina yote umewagawa wajumbe na wagombea wa nafasi hiyo, huku baadhi wakipongeza na wengine wakidai viongozi waliokuwa wanasimamia uchaguzi huo walishindwa kuendesha kiasi cha wajumbe kujiamulia muda wote.

Lyimo ameuponda uongozi uliokuwa unaongoza mkutano huo na kudai ulishindwa kusimamia katiba ya chama hicho kupunguza wagombea ili kupata majina ya watu watakaopigiwa kura.

"Viongozi wameshindwa kabisa kuzingatia katiba yetu, haiwezekana wapitishe majina yote, kama hivyo haikuwa na maana ya kufanya mkutano wa halmashauri kuu wenye jukumu la kuchuja wagombea," amesema Lyimo.


Mhandisi Aivan Jackson amepongeza kitendo cha wajumbe kupitisha majina yote yaliyowasilishwa na kubainisha timu Katibu Mkuu ambao wanasimamia uchaguzi huo walipanga kupitisha majina mawili tu.

"Nimepongeza ushujaa wa wajumbe kwakuwa na msimamo, kwani Katibu alitaka majina mawili yapite na wale walionekana wanaushawishi waenguliwe," amesema.

Hata hivyo, uchaguzi huo unafanyika leo Jumatatu, huku kukiwa hakuna Kamati ya kusimamia uchaguzi huo, huku viongozi wakidai wameshindwa kufanya hivyo kutokana na ukata wa kifedha.

Wanachama waliochukua fomu na kurudisha  walikuwa saba, lakini wengine wawili walijitoa dakika za mwisho kabla ya kuanza mkutano wa halmashauri kuu ambao ni Dominata Rwechangura na Kinanzaro Godfrey.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.