ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, February 16, 2023

WHO YAUNGANA NA WIZARA YA AFYA KUUNDA KAMATI ZA KUPAMBANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO KIBAHA.

 

Na Victor Masangu,Pwani


SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia,Wazee na watoto wameunda kikosi kazi maalum cha kupambana na magonjwa ya mlipuko hususani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini.

Kamati hiyo imeundwa jana kwa kujumuisha wataalam mbalimbali wakiwemo wa sekta ya afya, viongozi wa dini, viongozi wa kijamii,wawakilishi wa asasi zisizo za kiserikali,kamati ya ulinzi na usalama, waandishi wa habari na wadau wengine.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Idara ya Kinga Johnson Mlaki,amesema kuwa lengo kuu la kuunda kamati hiyo ni kuhakikisha jamii inapata uelewa kuhusu magonjwa ya mlipuko yanayotokea katika maeneo yao.

Mlaki ,amesema kuwa kamati hiyo itakuwa ikifanyakazi katika ngazi ya Wilaya ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya zikishirikiana na WHO ambao ndio wafadhili wakubwa hususani katika kutoa mafunzo mbalimbali kwa wajumbe wa kamati hiyo.
Amesema,majukumu ya kamati hiyo ni pamoja na kuelimisha jamii ,kufanya ufuatiliaji kwa kile kilichofanyika kuhusu magonjwa ya milipuko,kupokea,kutoa na kusambaza ujumbe mbalimbali kuhusu magonjwa ya mlipuko pamoja na kuzileta pamoja raslimali ambazo zitawasaidia wananchi.

Mlaki , ameongeza kuwa kwasasa tayari Wizara ya Afya imefanikiwa kuunda kamati hizo katika Mikoa minne ukiwemo Mkoa wa Pwani,Tanga,Geita,na Manyara lakini malengo yake ni kufika katika Mikoa yote nchini.

"Tumeanza na mikoa hii minne kwakuwa tumeona uchanjaji wa Covid -19 kwa baadhi ya Halmashauri ulikuwa chini na tuligundua sababu kubwa ni elimu kuwa ndogo lakini kwasasa tunahakikisha elimu inapanuka katika maeneo mengi zaidi,"amesema Mlaki.

Amesema,magonjwa ya milipuko ni mengi lakini yanayotisha zaidi ni pamoja na Covid -19,Ebola,Kipindupindu na Kimeta huku akisema Serikali kupitia Wizara imefanyakazi kubwa zaidi ya kupambana na magonjwa hayo.
Akifungua mafunzo ya siku moja ya kamati hiyo yaliyofanyika katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya  Kibaha Vijijini  Kaimu Afisa Tarafa ya  Mlandizi  Hamad Omary  ameishukuru Serikali  kwa kuunda kamati hiyo muhimu.

Omary,ametoa wito kwa wajumbe wa kamati hiyo kuhakikisha wanakwenda kufanyakazi kwa bidii ili kuepusha magonjwa ya mlipuko katika maeneo yao.

"Tunaishukuru Wizara ya afya pamoja na WHO kwa kutambua umuhimu wa kuunda kikosi kazi hiki kwa ajili ya kupambana na magonjwa ya milipuko hapa Kibaha Vijijini,ninahakika timu hii itakwenda kutoa elimu na kuhamasisha jamii namna ya kujikinga na magonjwa hayo,"amesema Omary
Hatahivyo,mwakilishi kutoka WHO Jaliath Rangi,amesema kuwa watashirikiana na kamati hiyo kila hatua na ikiwezekana kutoa mafunzo ya mara kwa mara ili kusudi tuweze kufikia malengo ya kukomesha magonjwa ya mlipuko.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.