Timu ya taifa ya soka ya Ufaransa imewasili nyumbani kutoka Qatar salama salmini na kupokelewa na umati mkubwa wa watu jijini Paris kwa mbwembwe.
Kikosi hicho kilikumbatiwa kwa shangwe na nderemo Jumatatu, Disemba 19, baada ya kushindwa na Argentina katika fainali ya Kombe la Dunia Jumapili, Disemba 18.
Deschamps na Hugo Lloris waliongoza timu hiyo wakifuatwa na fowadi pilipili Kylian Mbappé ambaye alifungia Ufaransa hat-trick katika fainali ambayo ilikuwa kubwa zaidi katika historia ya michuano hiyo.
Kisha wachezaji wengine walifuata wakiwa wamevalia tabasamu la ujasiri kuonyesha shukrani kwa maelfu waliojitokeza kuwapokea.
Licha ya kupoteza Kombe la Dunia, takriban mashabiki 50,000 walikusanyika katika Place de la Concorde ili kuwapa wachezaji wao makaribisho ya kifalme wakiachia fataki.
Hata hivyo, Mbappe alionekana kutojali na kununa baada ya kushuka kutoka kwenye ndege.
Alionekana kukasirika na kukata tamaa katika muda wote baada ya kukamilika kwa michuano hiyo ya kimataifa.
Meneja wake pia alionekana kumsaidia kuinua mkono wake ili kuwapungia mashabiki waliokuwa wakimsifu.
Makovu ya kushindwa Jumapili, yalikuwa bado hayajamtoka nyota huyo wa klabu ya PSG. Mbappe, ambaye alikua mchezaji wa kwanza baada ya Geoff Hurst kufunga hat-trick 1966, kwenye fainali ya Kombe la Dunia, ameapa kuwaa Ufaransa 'itarejea' tena. Juhudi zake, za kimiujiza kama zilivyokuwa, hazikutosha kusaidia upande wake kutetea taji lao.
Ufaransa ilisawazisha mara mbili katika fainali iliyomalizika kwa mabao 3-3, kabla ya Argentina kushinda kwa mikwaju ya penati 4-2.
Kuwasili kwao nyumbani kunajiri huku Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akikosolewa vikali kwa kuwafariji wachezaji baada ya kupoteza Kombe la Dunia.
Vyombo vya habari vya Ufaransa vilimkosoa mwanasiasa huyo namna alivyojaribu kumfariji Mbappe alipokuwa akibubujikwa na machozi katika uwanja wa Lusail Stadium.
Wakati huo huo, huku hatma ya kocha Deschamps ikiwa inayumba na kandarasi yake ikikaribia kumalizika, inaripotiwa kwamba anataka kufanya mazungumzo ya mkataba wake kurefushwa ili kusalia kuinoa timu ya Ufaransa kwa michuano ijayo ya Kombe la Dunia.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.