ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, November 17, 2022

MUSOMA, GEITA, UKEREWE KUPIGA MAKASIA KISHA FAINALI MBIO ZA MITUMBWI 11 DEC 2022 MWANZA

 NA ALBERT G. SENGO/MWANZA

ZAIDI ya wanamichezo 300 wanatarajiwa kushiriki mashindano ya mbio za mitumbwi yatakayofanyika katika mikoa ya Mara, Geita na Mwanza huku washindi wakiondoka na mamilioni ya fedha. Mashindano hayo yanayoandaliwa na The Scope Experience yanafanyika kwa mwaka wa 14 mfululizo yataanza wilayani Ukerewe Oktoba 27, Musoma Desemba 4 na fainali kuhitimishwa Desemba 11 jijini Mwanza katika eneo la Mwaloni (soko la Kirumba). Muandaaji wa mashindano hayo, Ayoub Sossy, amesema msimu huu wamepanua wigo na wanatarajia kufanya makubwa ambapo Musoma yatafanyika Kwenye mwalo wa Mwigobelo, Ukerewe (Monarch beach) na Mwanza (Mwaloni) kila kituo kutakuwa na wiki moja ya maandalizi na hamasa kwa wavuvi na wadau wengine lengo ni kuutambulisha mkoa na fursa zinazopatikana ili kuvutia wawekezaji na kufungua fursa za utalii. Meneja Mauzo wa TBL ambao ni wadhamini wa mashindano hayo, Yuda Ryaga amesema kila kituo kitashirikisha timu za wanaume na wanawake ambapo Ukerewe na Musoma washindi wa kwanza watapata Sh 500,000, wa pili Sh 300,000 na wa tatu Sh 200,000 kwa timu zote (Wanawake na wanaume). Amesema kwa upande wa fainali itakayofanyika Mwanza, kwa timu zote za wanawake na wanaume mshindi wa kwanza ataondoka na Sh 2 milioni, wa pili Sh 1.5 milioni na wa tatu Sh 1 milioni huku mshindi wa nne akipata Sh 800,000 na wa tano Sh 500,000 ambapo fedha hizo zitalipwa taslimu wakati wa mashindano. Naye Mwenyekiti wa mbio za Mitumbwi Mwanza, Ludovick Kanebuye amewataka wanamichezo wote waliosajiliwa kushiriki mbio hizo kwa kutumia vifaa (makasia na mitumbwi) ambayo imesajiliwa na mamlaka na kutambuliwa huku akisisitiza kila mtumbwi utakuwa na washiriki watano ambapo wanategemea zaidi ya wanamichezo 300 watashiriki.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.